Chama cha ACT Wazalendo kimemjibu Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa CPA. Amos Makalla, kikidai kuwa anapotosha ukweli kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakijiweki madarakani bali kinashinda kwa imani ya wananchi.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo, chama hicho kimeeleza kuwa CCM kilishapoteza imani ya Watanzania tangu zamani, na kwamba kimekuwa kikiendelea kushikilia madaraka kwa msaada wa vyombo vya dola.
“Makala akiwa wilayani Newala alitujibu ACT Wazalendo kuwa CCM hawajiweki madarakani na wanaendelea kushinda kwa sababu ya kuungwa mkono na wananchi. Tunaomba ndugu Makalla ajue kuwa CCM ni wezi wa uchaguzi, na wanatumia nguvu ya dola kusalia madarakani. Hali hiyo ndiyo inayosababisha chaguzi zetu kushindwa kuwa huru na za haki,” ilieleza taarifa hiyo.
ACT Wazalendo imesisitiza kuwa haitanyamaza, na itaendelea kutumia kila jukwaa kuwaelimisha na kuwaasa wananchi kuikataa CCM na kutumia haki yao ya kikatiba kuwaondoa madarakani kupitia sanduku la kura.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED