Wasira: Amani ndio nguzo ya maendeleo

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:15 PM Apr 17 2025
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Stephen Wasira
Picha: CCM
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Stephen Wasira

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Stephen Wasira, amesema ni muhimu kulinda amani ya nchi kwa kuwa ndani ya amani kuna haki, hasa haki ya wanyonge na wasiokuwa na sauti katika jamii.

Wasira ametoa kauli hiyo leo akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, ambako yuko katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM, huku akisisitiza kuwa amani ni msingi wa haki, maendeleo na ustawi wa jamii.

“Amani ikikosekana, wanaoumia zaidi ni wanawake, watoto na wanyonge. Ndani ya amani kuna haki. Huwezi ukaleta vurugu ukidhani unadai haki. Haki ya kweli hupatikana kwa njia ya amani na kufuata sheria,” amesema Wasira.

Amesema Tanzania imekuwa kimbilio la wengi kutoka mataifa jirani ambayo yalizokumbwa na migogoro, hivyo ni muhimu kwa Watanzania kulinda na kuthamini amani hiyo kama urithi wa vizazi vijavyo.


Pia amewapongeza viongozi wa CCM Mkoa wa Tabora kwa mshikamano wao mzuri na serikali, akieleza kuwa ushirikiano huo unasaidia kutatua changamoto za wananchi kwa haraka na kwa ufanisi.