Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Amson Group, Edha Nahdi, amekutana na Rais wa Kenya, William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, Aprili 18,2025 kwa ajili ya mazungumzo kuhusu uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa Kiwanda cha Saruji cha Bamburi Cement- awamu wa pili, wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 380 (Sh. bilioni 960).
Edha Nahdi, ambaye ana umri wa miaka 37, amefanikisha ununuzi wa Kampuni ya Bamburi Cement kwa thamani ya Sh. 500 bilioni (Dola za Marekani milioni 182), hatua iliyoandika rekodi kama uwekezaji mkubwa zaidi kufanywa na Mtanzania nje ya nchi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uwekezaji, uwekezaji huu unazidi ule wa mfanyabiashara Rostam Aziz, aliyewekeza nchini Kenya kupitia Kampuni ya Taifa Gas kwa Dola za Marekani milioni 130 (Sh. bilioni 338).
Mkataba wa ununuzi wa Bamburi Cement unatajwa kama uwekezaji mkubwa zaidi wa kibinafsi kutoka kwa kampuni ya Kitanzania nchini Kenya tangu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Uwekezaji huo unaimarisha nafasi ya Amson Group kupanua shughuli zake katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, Amson Group imeonesha nia ya kuwekeza zaidi nchini Uganda, baada ya Bamburi Cement kukamilisha uuzaji wa hisa zake kwa asilimia 70 katika kampuni tanzu ya Hima Cement kwa kampuni za Sarrai Group na Rwimi Holding, kwa thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 84 (Sh.bilioni 214) mnamo Machi 2024.
Amson Group, inayomilikiwa na familia ya Nahdi, inafanya biashara katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi, na sasa inatarajiwa kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji katika Afrika Mashariki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED