SAFARI YA KUMTUA MAMA NDOO; Ndoa iliyobomoka kwa shida ya maji

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 03:44 PM Apr 17 2025
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika halfa ya Wiki ya Maji, mwaka huu
Picha: Mtandao
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika halfa ya Wiki ya Maji, mwaka huu

BUGOGO ni kijiji kilichopo wilayani Shinyanga, ambacho wananchi wake walikuwa wakiishi wakikabiliwa na shida kubwa ya maji safi na salama.

Katika historia yao, watu hao walikuwa wakiteseka kupata huduma ya maji safi na salama, sababu walitegemea visima vya kienyeji vilivyokauka kila mara.

Hiyo inatokea, huku wanawake wakionekana ndio waliobeba mzigo mkubwa wa kuhakikisha familia zinapata maji ya matumizi ya kila siku.

Ukweli huo unaotolewa kwa namna ya uchungu na Flora Masanja, mkazi wa kijiji hicho ambaye simulizi yake inaonyesha namna athari za kukosa maji katika maisha ya kifamilia na kijamii.

Kimaisha, Flora ni mama wa watoto watano, ambaye maisha yake hayakuwa tofauti na kinamama wengine wa kijijini hapo, isipokuwa kwa mkasa mmoja mkubwa anaoutaja mkasa usiofutika katika maisha yake, ndoa yake kuvunjika kwa sababu ya kukosa maji kijijini humo. 

Anafafanua alikuwa anaamka usiku kwenda kijiji jirani kutafuta maji, hali inayomuingiza kwenye mgogoro na mume wake.

Kurejea simulizi yake, mumewe akajenga imani kwamba kuchelewa kurudi nyumbani, alikuwa akienda kuchepuka na wanaume wengine.

“Nilikuwa naamka saa 10 hadi 11 alfajiri, natembea zaidi ya kilomita tatu hadi kijiji jirani kufuata maji. Nikirudi nakuta mume wangu amekasirika akidai nilikwenda kuchepuka kwa wanaume. 

“Tuligombana sana mpaka mwaka 2011 akaamua kuondoka na kuniachia watoto,” anasimulia Flora. 

Mwanamke mwingine mwenye simulizi kama hiyo, Bahati Zengo, anasema shida ya maji kijijini humo, wanawake wengi walikuwa na migogoro katika familia zao.

Anataja, hiyo ni kutokana na wanaume kutokuwa na imani nao, kwa sababu wakifuata maji majira hayo ya usiku, wenza hao wanawashuku wanakwenda kukutana na wanaume wengine kimapenzi.

HALI YA MABADILIKO

Bahati huku akishukuru shirika binafsi liliilowaletea maji, akatamka: “Sasa hivi hakuna tena migogoro ya ndoa, wala vipigo kwa wanawake, kwa sababu maji yapo karibu!”

Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Bugogo Jiledya Shija, anakiri kabla ya kufika kwa mradi wa maji safi kijijini humo, wakahangaika kusuluhisha migogoro ya ndoa kila mara. 

“Ukosefu wa maji kijijini hapa tulikuwa tukipokea kesi nyingi za migogoro ya familia, kwa wanawake kutuhumiwa kuchepuka na wanaume kila wanapochelewa kurudi kutoka kuchota maji,” anaeleza Shija.

Anataja namna walisuluhisha kesi, akitaja njia za kimazungumzo, elimu na kuna mikasa ya mifarakano hadi ndoa kuvunjika, ikiwamo ya mwanamama Flora Masanja.

Nafuu ya upatikanaji maji inatajwa ilianza kuonekana mnamo Agosti 2022, wakati madai taasisi isiyo ya kiserikali ilipoanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika kijiji hicho cha Bugogo. 

Ni mradi uliokamilika Novemba mwaka jana, kwa gharama ya shilingi milioni 425.1, ukiwa na lengo la kuwapatia huduma ya majisafi na salama wananchi 2,584 wa kijiji hicho.

Kwa mujibu wa Devocatus Kamara, Mkurugenzi wa shirika lililoendesha mradi huo, umezinduliwa Machi 18, mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.

Akifafanua, mradi huo ni sehemu ya jitihada za shirika kuhakikisha jamii zinapata huduma za maji kwa karibu, hasa maeneo ya vijijini kunakosahaulika.

“Lengo la mradi huu ni kuwawezesha wakazi wa kijiji cha Bugogo, shule na zahanati kupata huduma ya majisafi na salama ndani ya umbali usiozidi mita 400,” anasema Kamara.

Anaendelea “ni sawa na wastani wa kutumia dakika 30 kwenda kwenye kituo cha kuchota maji na kurudi nyumbani na tumejenga vituo 14.”

Kamara anafafanua kuwa chanzo chake ni maji ya kisima kirefu chenye kina mita 115 na kina uwezo wa kutoa maji lita 12,000 kwa saa.

Anaeleza kwamba, wamejenga tangi lenye ujazo wa lita elfu 60 na mtandao huo wa maji urefu wake ni kilomita 19,479.

Anautaja kuwa mradi wameukabidhi kwa wananchi wenyewe kupitia Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO), ambao watauendesha pamoja na kuunganisha wateja wa majumbani.

 “Tunaamini kuwa maji ni msingi wa maendeleo, bila maji safi na salama hakuna afya, hakuna elimu, hakuna usawa wa kijinsia, na hakuna ustawi wa familia,” anafafanua Kamara.

Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum, anasifu hali ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wilayani Shinyanga unakwenda.

Anataja pia, kuwapo mradi unaoitwa Tinde Package, utakaozawadia vijiji 109 vitakuwa na majisafi na salama,

kati ya vijiji 126 vilivyopo wilayani humo, na kusalia vijiji 17 tu.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, anautafsiri mradi wa kijijini Bugogo una sura ya ukombizi kwa wanawake, akiwasihi wakazi hao wautunze, ili uwahudumie kwa ufanisi na muda mrefu, wasirudie shida ya maji.

Huku akiahidi serikali kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kutatua shida ya majisafi na salama kwa wananchi, serikali itajikita katika ajenda ya Rais Dk. Samia ya “kumtua ndoo kichwani mwanamke.”

JICHO LA RAIS

Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002, toleo la mwaka 2025 iliyozinduliwa na Rais Dk. Samia Machi 22, 2025 jijini Dar es Salaam, kwenye maadhimisho ya Wiki ya Maji, inasema ifikapo Desemba 2025, huduma za maji maeneo ya vijijini inapaswa kufika asilimia 85 na mjini asilimia 95.

Rais Dk. Samia akihutubia hadhira katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam siku hiyo, akasema maboresho kwenye Sera ya Taifa ya Maji ni lazima, kwa sababu inagusa sura pana.

Hapo anataja mambo kama ongezeko la watu nchini, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya siasa za dunia, akitaja kuwa hatua inayoleta maboresho ya huduma bora, pia majisafi na salama kwa Watanzania.

Akataja kuimarishwa usalama wa maji kwa kulinda na kutunza rasilimali za maji kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania katika namna endelevu na sio Wizara ya Maji pekee.

Kuendana na hilo, akaagiza kuanzishwa kwa Gridi ya Maji ya Taifa, kuwezesha uhakika wa maji nchini, kuwezesha maeneo yote kufikiwa na huduma ya uhakika ya maji kwa wakati wote.