Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imebaini uwepo wa shule zinazofundisha masomo ya sayansi bila kuwa na maabara, licha ya kuwa zimedahili wanafunzi ambao baadhi yao wanatarajiwa kufanya mitihani ya mwisho Mei 2025.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justin Nyamoga, wakati akisoma maoni ya Kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais –TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Nyamoga ameeleza kuwa Kamati inatambua kuwa mafanikio ya kufundisha masomo ya sayansi yanategemea uwepo wa maabara zilizo na vifaa kamili vya kufundishia na katika ukaguzi wa miradi mbalimbali ya shule za sekondari nchini, Kamati iligundua kuwa baadhi ya shule hazina vifaa vya maabara kabisa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati, asilimia kubwa ya shule hizo tayari zimekwishadahili wanafunzi, huku baadhi yao wakitarajiwa kufanya mitihani ya mwisho Mei mwaka huu wa 2025.
“Kamati inahofia kuwa wanafunzi hao, kama Serikali haitakuwa na mpango wa dharura, watafanya mitihani yao bila uwezo wa kufanya mafunzo kwa vitendo (practical) kutokana na kutokuwepo kwa maabara,” ameongeza.
Kutokana na hali hiyo, Kamati imeshauri Serikali kuweka mpango wa dharura wa kupeleka vifaa vya maabara kwenye shule zote 26 za wasichana za mikoa bila kuathiri mipango ya kupeleka vifaa hivyo kwenye shule nyingine za sekondari.
“Kwa kuwa tatizo la uhaba wa vifaa vya maabara katika shule za sekondari nchini ni la muda mrefu na linaonekana kuwa gumu, Kamati inashauri Serikali itenge fungu maalumu kwa kutumia chanzo maalumu na cha kudumu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari nchini wakati wote vinapohitajika,” amesema Nyamoga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED