Waziri Kikwete aelezwa PSSSF Kidijitali ilivyopokelewa na wanachama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:19 PM Apr 28 2025
Meneja wa PSSSF Mkoa wa Singida, Beda Mgonja, akimueleza Waziri Kikwete jinsi PSSSF Kidijitali ilivyopokelewa na wanachama.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja wa PSSSF Mkoa wa Singida, Beda Mgonja, akimueleza Waziri Kikwete jinsi PSSSF Kidijitali ilivyopokelewa na wanachama.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ametembelea banda la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye kilele cha Maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwenye viwanja vya Mandewa mkoani Singida Aprili 28, 2025.

Katika banda la PSSSF, Kikwete alipokelewa na Meneja wa PSSSF Mkoa wa Singida, Beda Mgonja, ambaye alimueleza kuwa pamoja na kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wanachama na wananchi, Mfuko ulijikita katika kuhamasisha na kutoa elimu kwa wanachama kuhusu matumizi ya Mfumo wa utoaji huduma kwa njia ya Mtandao maarufu PSSSF Kidijitali.

Aidha, Afisa Mkuu wa Uhusiano PSSSF, Abdul Njaidi, alimueleza Waziri kuwa matumizi ya PSSSF Kidijitali yamepokelewa kwa furaha na wananchama na yameleta mapinduzi makubwa katika utoaji huduma ambapo mfumo huo umeondoa matumizi ya karatasi na kuondoa usumbufu kwa wanachama kufuata huduma.

Akitoa ushuhuda kuhusu mfumo wa PSSSF Kidijitali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda alimueleza Waziri kuwa, yeye alijiunga na Mfumo huo wa PSSSF Kidijitali jana (Aprili 27, 2025) na amefurahishwa na jinsi mfumo huo unavyoakisi kauli mbiu ya Maonesho “Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia ya Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahali pa Kazi.”