Ukitupa mtoto faini mil.5/- au kifungoni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:27 PM Apr 28 2025
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Mwanaidi Ali Khamis
Picha: Mtandao
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Mwanaidi Ali Khamis

Serikali imesema mwanamke atakayebainika kutupa mtoto atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo faini isiyopungua Sh.Milioni tano, kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Mwanaidi Ali Khamis ameyasema leo bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza, Mbunge wa Mwera (CCM), Zahor Mohamed Haji ambaye amehoji serikali haioni ipo haja ya kuboresha sheria ili kuwa kali kudhibiti matukio ya utupaji watoto.

Mwanaidi amesema serikali inakemea na kulaani kitendo cha baadhi ya wanawake kutupa watoto kwa lengo la kukwepa jukumu lao la msingi la kusimamia malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

Hata hivyo, amesema jamii itambue kuwa serikali itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya wanawake watakaokutwa na hatia ya kutenda kosa hilo na kuadhibiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 pamoja na Sheria nyingine za nchi zinazopinga suala hilo.

Amewasihi wale wanaoshindwa kutekeleza jukumu la malezi ya mtoto basi watoe taarifa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hususani Ofisi za Ustawi wa Jamii ambao watawajibika kuweka mpango wa huduma mbadala kwa Mtoto husika sawa na matakwa ya kifungu Na.94(5) cha Sheria ya Mtoto Sura ya 13.