MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,ametoa Shilingi milioni 3 kuunga mkono michezo ya jadi, inayotarajiwa kufanyika katika Manispaa ya Shinyanga.
Michezo hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 29 hadi Mei 2, 2025, ikihusisha kata 12 za Manispaa ya Shinyanga. ambapo Katambi ndiyo mfadhili mkuu wa michezo hiyo itakayo gharimu Sh.milioni 6.3 na sasa amekabidhi milioni 3.
Fedha hizo zimekabidhiwa jana na Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Hamisa Chacha, kwa niaba ya Mbunge Katambi, katika ofisi za chama hicho. Akizungumza wakati wa makabidhiano, Hamisa amesema michezo ya jadi ni muhimu katika kudumisha mila, tamaduni na maadili ya Mtanzania, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya maeneo yameanza kusahau kabisa mizizi yao ya kiafrika.
“Michezo hii ya jadi ni muhimu sana hasa katika kulinda maadili ya Mwafrika, sababu kuna maeneo mengine yameanza kusahau kabisa Maadili ya kiafrika,” amesema Chacha.
Aidha,amesema kuwa michezo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kumpongeza Mbunge Katambi kwa kuendelea kutekeleza ilani hiyo kwa vitendo. Amewapongeza pia waandaaji wa michezo hiyo ya Jadi, kwamba watawakutanisha watu pamoja na kuenzi Mila na Tamaduni zao.
Mwenyekiti wa Michezo ya Jadi wa Manispaa hiyo, Janeth Seseja, ametoa shukrani kwa Mbunge Katambi kwa kujitolea na kukubali ombi lao, akisema kuwa fedha hizo zitasaidia kufanikisha maandalizi ya michezo hiyo,huku akimuomba aendelee kuwa na moyo huo huo wa kujitoa kwa jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED