Mruma wa basi la Mvungi, akana mashtaka 29 ajali ya Ugweno

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 04:21 PM Apr 26 2025
Ilivyokuwa ajali ya basi la Ugweno Aprili 3 mwaka huu.
PICHA: MTANDAO
Ilivyokuwa ajali ya basi la Ugweno Aprili 3 mwaka huu.

DEREVA wa Basi la Kampuni ya Mvungi, linalokuwa likifanya safari zake kati ya Ugweno-Mwanga na Dar es Salaam, Al-Adani Mruma (47), anayedaiwa kusababisha ajali iliyoua watu saba na wengine 42 kujeruhiwa, amekana mashtaka 29 yanayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Moshi.

Ajali hiyo iliyotokea Aprili 3 mwaka huu, majira ya 12:45 asubuhi katika Kijiji cha Mamba, Kata ya Msangeni, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, ilisababishwa na uzembe wa dereva, uliotokana na kushindwa kulimudu gari, wakati akipishana na gari jingine kwenye kona kali na kuacha barabara na kutumbukia bondeni.

Mruma, alifikishwa jana (23 Aprili 2025) katika mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Ally Mkama na kusomewa mashtaka hayo ikiwemo kusabisha vifo, kuharibu mali na kusababisha majeraha kwa abiria.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Julieth Komba, anayesaidiwa na Bertina Tarimo, mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa hayo, Aprili 3, 2025 huko katika Kijiji cha Mamba, barabara ya Ugweno, Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro, akiwa dereva wa basi la abiria lenye namba za usajili T 222 DNL, aina ya Yountong.