FAHAMU KWA KINA MARADHI YA MOYO KUSHINDWA KUFANYA KAZI

By Daktari Dk. Mabula Budodi , Agency
Published at 12:25 PM Apr 27 2025
Mfumo wa moyo
Picha: Mtandao
Mfumo wa moyo

Kushindwa kwa moyo ni changamoto/hali ambayo inawakumba watu wengi sana duniani lakini bado uelewa ni mdogo sana juu yake.

Mara nyingi hukosewa na kuufafanisha na mshituko wa moyo, Kushindwa kwa moyo ni hali ambayo moyo hushindwa kufanya kazi yake ya kusukuma damu mwilini vizuri ambayo mwisho wake huweza kuleta changamoto nyingine za kiafya mwilini.

Pamoja na maendeleo ya afya na vifaa tiba duniani, kushindwa kwa moyo kumeendelea kuwa moja ya sababu ya watu wengi kulazwa hosipitalini na hata kuishia kwenye vifo vya wagonjwa hao, hivyo uelewa wa jambo hili na kujikinga ni jambo muhimu sana kwa watu wote.

Kushindwa kwa moyo si kwamba moyo wako haufanyi kazi tena au umesimama, la hasha! Ni kwamba moyo wako hauwezi kusukuma damu vizuri mwilini kama inavyotakiwa.

Hali hii ya kushindwa kwa moyo huweza kutokea kwa mtu yeyote kwa ghafla au kwa muda mrefu yaani kuwa na hali ya usugu.

Watu wazee wana uwezekano mkubwa wa kuwa na matatizo mengine ya moyo ambayo yanaweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi.

Lakini kuna wale ambao wamezaliwa na changamoto ya moyo tayari na hata kupata changamoto ya moyo kama ya vali za moyo ambayo huweza kupelekea kupata changamoto za moyo.

Kuna aina mbili tofauti za kushindwa kwa moyo. Aina ya kwanza ni kushindwa kwa moyo kunakohusiana na upungufu wa usukumaji damu kutoka kwenye moyo kwenda mwilini, kiwango cha damu kutoka moyoni kinapungua. 

Hii husababishwa na misuli ya moyo kudhoofika, hivyo kushindwa kusukuma/kupampu damu vizuri.

Aina ya pili ya kushindwa kwa moyo ni hali ya moyo, una uwezo wa kusukuma damu vizuri lakini misuli ya moyo imekakamaa kiasi kwamba haiwezi kuvutika na kujaa vizuri damu ya kutosha kwa ajili ya kusukumwa kwenda mwilini.

DALILI ZAKE

Kushindwa kwa moyo ni jambo la usugu la mwendelezo, hivyo watu wengine hushindwa kutilia maani dalili mpaka zinapokuwa kali maana huja kwa kukusanyika na dalili hizi huweza kuwa:

Kushindwa/kupungukiwa kupumua katika shughuli ya kutumia nguvu kama kupanda ngazi, kufanya mazoezi ya kukimbia na kutembea kwa haraka 

Kupungukiwa pumzi wakati wa kulala chini, yaani ukiwa umenyooka mfano kitandani na kupata ahuweni ukiwa umekaa.

Kukohoa kikohozi kikavu kisichoisha na hata filimbi za miruzi kwenye kifua wakati wa kupumua

Mwili kuchoka na kudhoofu kuliko kawaida na kila wakati, muda mwingi bila hata kufanya shughuli yoyote.

Kuvimba miguu, tumbo au mwili mzima kufuatana na hali ya kushindwa kwa moyo wako kumefikia.

Kuongezeka uzito sana kwa ghafla. Ni mwanzo wa kupata tatizo hili, lakini pia kupungua uzito sana na kupoteza mafuta na misuli kudhoofu hata pale unapokula chakula cha kutosha.

Kupungua uwezo wa kufanya mazoezi kama siku zote ulikuwa unaweza kufanya.

SABABU ZAKE

Mambo tofauti huweza kupelekea kushindwa kwa moyo. Sababu hizi hujumuisha:

Magonjwa ya mishipa ya damu kama kuwa na mafuta ya rehemu nyingi kwenye mishipa ya damu hii hupunguza ukubwa wa mishipa ya damu ambayo huishia kudhoofisha misuli ya moyo.

Shinikizo la damu kwa muda mrefu hufanya moyo kufanya kazi kwa nguvu sana hivyo hupelekea kutanuka sana na kuharibika.

Kisukari huchangia kuharibu mishipa ya damu hivyo kupelekea kupata magonjwa ya moyo.

Unene uliopitiliza na mfumo wa maisha ya kutokuwa na mazoezi kabisa huchangia kuweka uzito na kazi ya ziada kwenye moyo na kukosa mazoezi hudhoofisha moyo.

Mambo mengine huchangia shida hii kama kunywa pombe kupita kiasi, kuvuta sigara n.k.

NAMNA YA KUZUIA 

Kuna mambo kadhaa kama vinasaba vya mwili ambavyo haviwezi badilika na huwa vinachangia kupata shinikizo la damu, lakini kuna baadhi ya mambo huweza kufanyika kutengeneza mazingira mazuri ya afya ya moyo wako kama:

Kufanya mazoezi mara kwa mara kama vile kutembea, huimarisha afya ya moyo.

Kula chakula rafiki cha moyo na kupunguza vyakula vya chumvi nyingi, kuacha vyakula vyenye mafuta mengi, kupunguza vyakula vya kusindikwa. Huchangia kupunguza urundikanaji maji mwilini hata kukabili shinikizo la damu.

Zingatia matumizi ya dawa za moyo, kutumia dawa za moyo ulizoanzishiwa huweza kulinda moyo wako usiendelee kuharibika hata kushindwa kufanya kazi kabisa, hivyo zingatia matumizi ya dawa ulizoanzishiwa.

Zingatia kuchunguza afya yako mara kwa mara kama mtakavyopanga na daktari wako.

Familia kuwa karibu na mgonjwa wa moyo kumpa msaada kutokana na changamoto ya mgonjwa huyo kwa kuwa kutokana na kushindwa kwa moyo, muda mwingi hujiona kama amepungukiwa sana.

Tafadhali zingatia ushauri wa dakitari wako.