Hatimaye Benki Ushirika rasmi mwezi huu, kipaumbele mkulima

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:04 PM Apr 28 2025
Wanaushirika katika moja ya maandamano
Picha: Maktaba
Wanaushirika katika moja ya maandamano

MOJA ya nguzo muhimu zenye hisitoria kuinua uchuki wa nchi, haswa kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo (1969 hadi 1974) vilikuwa vya ushirika nchini.

Ni vyombo nchini sasa vina mchango muhimu katika uchumi wa nchi, hasa kuwawezesha wananchi kushiriki kwa pamoja katika biashara na kuongeza mapato yao. 

Hadi sasa mitaani ishara yake iko pale vinaposhudiwa vyombo vya ‘Vicoba’ na SACCOS, vinaangukia huko, huku zamani kuna ishara za kihistoria ‘maduka ya ushirika.’ 

Ni vyama vinavyosaidia wanachama na hasa wakulima, kupata masoko, kushiriki katika huduma za kifedha, kuboresha maisha yao ya kiuchumi. 

Katika nchi nyingi zinazoendelea, vyama vya ushirika vimekuwa na jukumu kubwa ya kuunganisha nguvu ya wanachama, kuboresha teknolojia ya uzalishaji, na kuongeza ushawishi wa pamoja katika soko. 

Licha ya umuhimu wake, kwa sasa vyama vya ushirika vinakabiliwa na changamoto zinazoweza kuathiri ufanisi wake, hata kukwamisha kufikia malengo yake, ikiwamo ukosefu wa mitaji na rasilimali kifedha za kujiendesha. 

Wanachama wengi wa vyama  ushirika kwa sasa ni wakulima wadogo, wasio na uwezo mkubwa wa fedha kutoa michango mikubwa ya kuimarisha vyama vyao.

Hiyo inatakwa kusababisha vyama vya ushirika kushindwa kununua vifaa vya kisasa, kuboresha huduma zao, na kupanua shughuli za uzalishaji.

SERIKALI YAJITOKEZA

Baada ya changamoto hizo za muda mrefu, serikali imekuja na suluhisho lao kuanzisha benki maalumu inayotarajiwa kusaidia kutatua shida hizo, hususani katika eneo la mitaji ya kuendeleza uwekezaji.

Fares Muganda, ni Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), anasema benki hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Aprili 28 mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan, na makao yake ni Dodoma.

Muganda anafafanua kwamba itahudumia wateja wote, ila lengo lake kubwa ni kwa wana- ushirika ambao ndio wamiliki wake kwa asilimia 51.

Anasema nchini kuna vyama vya ushirika zaidi ya 6,000 vilivyosajiliwa, vikiwa na wanachama zaidi ya milioni 10. Hiyo ni sawa na kuwagusa Watanzania wasiopungua asilimia 16.

Muganda Anasema malengo yao ni kwamba mpaka kufikia mwaka 2030 wawe wamefikia zaidi ya wateja milioni 10 na itakuwa benki ya kipekee.

Anataja malengo mengine yaliyowekwa na serikali ya kuhakikisha mkulima anaongezeka kiuchumi yanatekelezeka.

Anasema sababu ya benki hiyo kuanzishwa, ni baada ya kuonekana ombwe lililopo kwa wakulima na kwamba safari ya kuitafuta kuanzishwa kwake haikuwa rahisi.

Anasema mipango ya kuanzishwa kwake ilianza mwaka 2012.

 KUTOKA BENKI

Yahya Kiyabo, ni Mkuu wa Idara na Ushirika kutoka Benki ya Ushirika, anasema wakulima wengi nchini wamekuwa wakikosa mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao kwa kuwekewa vikwazo kwamba hawakopesheki lakini sasa wanakwenda kuwatengenezea mfumo wa kuwapatia mikopo.

Anasema benki hiyo italenga kuwahudumia wakulima zaidi ambao ndio wana- ushirika wenyewe.

Pia, anasema asilimia ndogo ya huduma itatolewa kwa wateja wengine.

“Kwa maana tunaangalia pia kwa wamama, vijana na sehemu kubwa ambao waliachwa sana katika mjumuisho wa kifedha. Tunajipambanua kuja na huduma ambazo zinaendana na sekta ya ushirika zaidi,"anasema Kiyabo.

Anasema mitazamo iliyozoeleka awali kwamba ‘wakulima hawakopesheki’ ni kwa sababu hawakutengenezewa mazingira mazuri wakopesheka.

"Kwa sasa tunasema sisi tumekuja na tutawaandaa na tutawaweka kwenye rekodi. Tunaanza kumsajili mkulima, tunamwingiza kwenye ‘database’ (takwimu) yetu.

“Kwa hiyo, atakuwa kwenye historia yetu, ili hata ikifika kipindi ameuza na tuna uhakika atalipwa, tutampatia malipo ya awali wakati anasubiri mnada ufanyike.

"Atapata fedha yake baadae, kwa hiyo ndiyo hivyo vitu vinavyokuja kumsaidia mkulima na ndiyo maana tunataka tuanze naye toka mwanzo, pia kwa sababu atakuwa kwenye database yetu, tutamwekea mfumo maalumu wa malipo.

"Mkulima ni mfanyakazi kama ilivyo kwa mwingine, kwa sababu kama ana uwezo wa kupata kipato chake cha Sh. milioni 70 au 80 kwa mwaka, ukijaribu kuigawanya hiyo ni kipato ambacho mtumishi anapata kila mwezi.

“Kwa hiyo, tukiwa na database kama hiyo tunaweza ‘kum-advance’ (kumpatia kwanza) mkulima na tukawa na uhakika kwamba muda ukifika wa mazao ataturejeshea fedha yetu."

Anataja kuwapo makundi mengine, lakini kipauambele ni wana – ushirika, akinena ushirika umesaidia mataifa mengi kusukuma uchumi wake.

MIPANGO YA MKULIMA

Kiyabo anasema: ““Tunataka tuanze kumsaidia mkulima siyo mpaka tusubiri amevuna, tunataka tuanze kumsaidia mkulima kuanzia kwenye taratibu za kuandaa shamba mpaka anapopeleka mzigo wake kwenye chama cha msingi.

Anasema Watanzania ambao wamefikiwa na huduma ya kifedha ni asilimia 22 pekee, hivyo kuna pengo la asilimia 78 wasiofikiwa na huduma hizo na kwamba ndio maana wameamua kuanzisha benki hiyo ambayo ndio imeanzia vijijini.

 “Tunataka kufikia mwaka 2030, Benki ya Ushirika iwe imechagiza kwa asilimia 50 ya kuwafikia wananchi kwa huduma ya kifedha.

“Tunataka mkulima kuanzia kule kijijini ajue ni namna gani ya kutumia benki hiyo, na vyama vya ushirika vitakuwa ni sehemu ya mawakala wa benki, ili wakulima wapate huduma za kibenki wakiwa hukohuko waliko."

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania, Muganda, vyama hivyo ni vyombo vya kiuchumi vilivyoanzishwa kwa wakulima, lengo ni kuwaleta pamoja kama sehemu ya kuleta mazao na kuyauza.

Kwamba, Ushirika unawasaidia kutafuta na kupata soko zuri ili wapate bei ambayo itaendana na kazi kubwa wanayoifanya kwenye shughuli za ukulima.

“Kwa hiyo, sisi kama shirikisho kazi yetu kubwa ni kuvisimamia vyama vyote hivyo, kwanza katika kuvisemea, kufuatilia mambo ya kisera, kuhakikisha kwamba sheria zote zinazotungwa chini ya Bunge la Tanzania na maelezo na kanuni zote zinazohusiana na masuala ya kilimo, yanatekelezwa...

“Lakini pale ambapo kunakuwa na changamoto, sisi ndio tunatakiwa kuyaleta mawazo kwa serikali kwa kupitia ngazi zilizopo, kunzia ngazi za mkoa mpaka kitaifa na kuhakikisha mambo haya yote yanazungumzika na sera zinazotungwa,” anasema.