MIAKA 32 iliyopita, Simba SC walifika fainali ya michuano ya Afrika (CAF Cup Winners' Cup) mwaka 1993, wakapambana vikali dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast lakini wakateleza. Kilio hicho hakikuwahi kufutika; kiligeuka kuwa deni lililodumu kizazi hadi kizazi.
Mwaka 2025, Simba SC wameandika sura mpya: kufuzu tena fainali ya CAF Confederation Cup, na sasa wamepewa nafasi ya kulipa deni hilo la kihistoria. Safari hii, siyo tu kwa ajili yao, bali kwa vizazi vyote vilivyoamini katika ndoto hiyo kwa miongo mitatu.
Katika kila pambano, Simba SC wamejiandalia njia ya ushindi kwa ujasiri na bidii isiyo na kifani. Sio tu kwamba wamekimbia mbali na vikwazo vya kila aina, bali wamejionyesha kuwa na damu ya mabingwa.
Kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup) mwaka 2025 ni ushahidi wa wazi kuwa wana nafasi ya kubeba taji la Afrika, ukiwa kwenye nafasi ya aina hii, unatazamwa kama bingwa mtarajiwa. Lakini, je, wameshafanya kile kinachohitajika ili kuwa mabingwa hata kabla ya fainali?
Safari ya jasho na damu
Simba SC ilianza safari yake katika Kundi A, maarufu kama "Kundi la Kifo", pamoja na timu kubwa kama CS Sfaxien ya Tunisia, CS Constantine ya Algeria, na Bravos do Maquis ya Angola.
Ingawa kundi hili lilikuwa na timu kubwa na ngumu Afrika, Simba walijenga msingi wa ubingwa kwa kuonyesha soka la kiwango cha juu, wakiongoza kundi na kupata matokeo ugenini kwa CS Sfaxien. Hii ni tabia ya mabingwa kushinda ugenini.
Katika robo fainali, walikumbana na changamoto kubwa, ugenini walifungwa 2-0 na Al Masry huko Misri, lakini walirudi Benjamin Mkapa Stadium, Dar es Salaam walipindua matokeo kwa kushinda 2-0, na kwenda kwenye penati na kushinda kwa penati 4-1.
Katika nusu fainali, licha ya kumaliza mechi ya kwanza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Stellenbosch FC pale Zanzibar, Simba walikutana na changamoto kubwa ugenini Durban. Huku wakicheza chini ya kiwango, na uwanja uliokua na changamoto, walipata sare ya 0-0 na kufuzu fainali. Hali hii inadhihirisha ubingwa wa Simba; ni timu inayoweza kupambana kwa ustahimilivu na kufikia malengo hata katika hali ngumu.
"Haikuwa kazi rahisi sababu mpango wetu ilikuwa kupata goli mapema", anasema Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola
Hatua za juu za mabingwa
"Tumefanikiwa kufikia hatua ambayo tulikuwa tunatamani tuifikie tena na historia yetu tumecheza (fainali) mwaka 1993, lakini miaka 32 baadaye tumeweza kufanikiwa", anasema Murtaza Mangungu mwenyekiti wa Simba akipongeza Wachezaji na benchi la ufundi.
Simba imefika fainali ya CAF kwa mara ya pili baada ya ile ya awali mwaka 1993. Ukiacha fainali, imeshawahi kutinga nusu fainali nyingine ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa) mwaka 1974.
Aidha Simba imekuwa na tabia ya kufika hatua za juu mara kwa mara hasa Robo fainali. Tangu mwaka 2018 hadi sasa, Simba SC imefanikiwa kuwa klabu yenye mafanikio makubwa zaidi kimataifa kutoka Afrika Mashariki kwa kufika robo fainali sita katika mashindano makubwa barani Afrika. Na sasa imetinga Fainali baada ya kuitoa Stellenboch ya Afrika Kusini.
Hatua hizi hawaingii timu za kawaida, huingia mabingwa au timu zenye sifa ya ubingwa. Simba imefanya hivyo, inaweza kuwekwa kwenye kapu la mabingwa.
Fedha na heshima
Kupitia hatua hii ya fainali, Simba SC wamepata zawadi kubwa ya kifedha, wakikusanya dola milioni moja kwa kufika hatua hii ya juu. Na iwapo itashinda ubingwa itapata dola milioni 2. Hii si tu ni faida ya kifedha, bali ni ushahidi wa ubingwa wao wa kweli. Ni timu mabingwa huwania ama hupata pesa kiasi kikubwa hivi, na Simba wamejiweka katika nafasi hiyo.
Zaidi ya pesa, Simba SC wamejikusanyia heshima kubwa kwa bara zima la Afrika. Rais Samia Suluhu akiipongeza kwa kufika fainali kupitia mtandao wake wa twitter ameandika: "mmeipa nchi yetu heshima kubwa. Nawatakia kila kheri. Mnayo hamasa yangu wakati wote".
Hata baada ya mechi ya nusu fainali, kule Afrika Kusini, kocha wa Stellenbosch, Steve Barker alikaririwa hadharani akisema: "Simba ni timu kubwa Afrika." Hii ni ishara kwamba Simba wamejijengea heshima ya dhati, na wanayo mafasi ya kuendelea kujenga heshima katika soka la Afrika.
Simba wameonyesha siyo tu kwamba wana uwezo wa kushinda, bali pia wanajitahidi kudumisha ubingwa na heshima yao kwa kila hatua wanayochukua.
Ubora na viwango Afrika
Maelezo ya picha,Simba imeitoa Stellenbosch kwa jumla ya bao 1-0, baada ya sare ya 0-0 Durban na kutinga fainali ya CAF
Kwa mujibu wa viwango vya CAF, Simba SC sasa inashika nafasi ya 4 bora barani Afrika, nyuma ya Al Ahly, Mamelodi Sundowns, na Espérance de Tunis. Hii ni ishara ya nguvu ya Simba, ambao sasa wanatajwa kwenye miongoni mwa timu bora kabisa kwenye soka la Afrika. Kuwa tano bora kwa viwango Afrika ni nafasi za mabingwa sio kila timu inaweza kuwa kwenye nafasi hiyo.
Kwa kupambana na timu kama CS Sfaxien ya Tunisia, CS Constantine, Al Masry na kuindoa Stellenbosch na kutinga fainali nyingine ingawa ni baada ya miaka mingi, Simba SC imeonyesha kwamba ni klabu inayoweza kupambana na vigogo wa Afrika. Hii ni hatua muhimu si tu kwa klabu bali pia kwa ligi ya Tanzania kwa ujumla, ambayo inakuwa na heshima na kuimarika kwa kiwango cha juu kwenye soka la Afrika.
Kupanda kwa viwango vya Simba ni hatua muhimu katika kupandisha hadhi ya ligi ya Tanzania kwa viwango vya kimataifa. Hutashangaa orodha mpya ya viwango vya ligi bora Afrika, ligi ya Tanzania itaendelea kuwa miongoni mwa ligi tano bora Afrika. Mchango wa Simba huwezi kuupuuza. Ni mabingwa tu husaidia ligi zao kupanda kwenye orodha ya viwango. Kwa ujumla, Simba SC wamekuwa nguzo ya ufanisi na mchango mkubwa kwa soka la Afrika Mashariki na Tanzania.
Je, ubingwa huu unatosha?
Simba SC wamejionyesha kuwa mabingwa hata kabla ya kushinda fainali, kwa kujizatiti, kupambana kwa ustahimilivu na kuvivimbia vilabu vikubwa kwa kila hatua waliyopita. Wamejijengea hadhi ambayo haitaweza kupingwa tena na wameweka historia. Hadhi ya kuheshimiwa ya kutinga fainali kama walivyofanya watani zao Yanga misimu miwili iliyopita.
Hata hivyo hadhi ya ubingwa wa aina hii na hatua waliopo sasa haitoshi. Wanapaswa saaa kupiga hatua moja mbele ya kutwaa kombe la Afrika.
Si rahisi lakini inawezekana. Wanayo nafasi hivyo wakitarajiwa kucheza na RSB Berkane wakianzia ugenini Mei 17, 2025 na kumalizia nyumbani Mei 25, 2025.
Kocha wao Davids Fadlu analiona hilo na anasema hawapaswi kufurahia sana hatua hii, wanapaswa kujielekeza kwenye kotwaa kombe akiungwa mkono na nahodha wake Mohamed Hussein.
"Hii hatuishii hapa, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu inshallah tunakwenda kuchukua taji hili", anasema nahodha.
Ni sahihi ni wakati wa kushinda kombe ili kuthibitisha kuwa ni mabingwa wa makombe na hawakufika hatua hii kwa bahati.
BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED