CHAMA cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA), kimeitisha Mkutano wake wa Halmshauri Kuu kesho, huku tetesi zilizopo ni kwamba huenda ni cha kuwapokea waliohama kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) maarufu kama G55.
Akizungumza na Nipashe, Mwenyekiti taifa wa chama hicho, Hashim Rungwe, alithibitisha kuitisha kikao hicho licha ya kushindwa kuweka wazi agenda za kikao hicho.
Hata alipoulizwa kuhusu endapo kikao hicho kitatumika kuwapokea G55, alikataa.
“Ni kweli kesho tutafanya kikao cha Halmashauri Kuu, lakini agenda, tutajua hukohuko na mahali tutakapofanyia tutawajulisha baadae,”amesema Rungwe.
Taarifa ambazo Nipashe inazo ni kwamba, siku za hivi karibuni, chama hicho kimekuwa na vikao mfululizo kila siku lakini viongozi wa chama hicho walipoulizwa, walisema ni kwa ajili ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.
“Ni vikao vya kawaida vya chama, lakini kama unavyojua huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu, hivyo ni lazima mjipange.”
Ikumbukwe kwamba, baadhi ya wanachama waliohama CHADEMA, wamekuwa wakitajwa kwamba huenda wakahamia kwenye chama hicho cha CHAUMMA.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED