EWURA: Tathmini ya bei mpya umeme yaja mwakani

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:11 PM Apr 28 2025
•	Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipotembea moja ya mitambo ya kuzalisha umeme nchini
Picha: Mtandao
• Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipotembea moja ya mitambo ya kuzalisha umeme nchini

APRILI 9, 2025, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ilizindua Ripoti za Sekta ya Nishati (umeme, mafuta na gesi asilia) kwa mwaka 2023/24, ikianika undani wake.

Katika ripoti hiyo, sekta ndogo ya umeme imeonekana kukua ikichangia zaidi kiuchumi na kijamii, huku mahitaji ya umeme yanakadiriwa kukua kwa asilimia 11.7 kila mwaka. 

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, anasema uzalishaji umeme uliongezeka kwa megawati 499.9 sawa na asilimia 26.15. Ni kutoka megawati 1,911.46 za mwaka 2022/2023 hadi 2411.33 mwaka 2023/24.

Anasema mahitaji yake yaliongezeka kwa megawati 174.73 sawa na asilimia 11.88. Mahitaji yalitoka megawati 1,470.50 mwaka 2022/2023 hadi 1,645.23 mwaka 2023/2024. 

MIAKA IJAYO

Anasema ukuaji huo unakadiriwa kuongeza mahitaji ya umeme hadi megawati 2,677 kwa mwaka huu; megawati 4,878 (2030), megawati 8,554 (2035); megawati 12,854 (2040); na 17,611 (2044).

Pia, anasema kuongezeka mahitaji ya umeme, uzalishaji wake pia unatarajiwa kuongezeka. Inakadiriwa kuwapo megawati 2,677 mwaka 2025; megawati 4,878 (2030), megawati 8,554 (2035), megawati 12,854 (2040), na megawati 17,611 (2044).

GHARAMA ZA UMEME

Dk. Andilile anasema mwaka ujao wa fedha watafanya tathimini ya gharama ya huduma, baada kubaini bei hazijarekebishwa tangu mwaka 2016.

Pia, anasema uamuzi wa serikali  kuacha mitambo ya kukodi iliyokuwapo huko nyuma, bei za umeme zilipanda kwa takribani asilimia 40 mwaka 2011 na asilimia 39 mwaka 2013.

Anasema TANESCO imeendelea kuimarika kutokana na bei umeme kuoongezwa, pia uamuzi wa serikali kukabili deni lililokuwapo la takribani Sh.Trilioni 2.4, imekuwa msaada.

VITUO MAFUTA VIJIJINI 

Anasema hadi kufikia Juni 30, 2024, vituo vya mafuta vilivyopo vijijini nchini vimeongezeka kwa asilimia 32.96, kutoka vituo 361 hadi vituo 480. 

“Hii inaashiria juhudi kubwa za kuimarisha upatikanaji wa huduma za mafuta katika maeneo ya pembezoni, kuongezeka kwa uwekezaji huu kumetokana na mahitaji makubwa ya mafuta nchini,” anasema Dk. Andilile,

Anaendelea: “Ukuaji wa shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, madini, na ujenzi, uongezekaji wa shughuli za usafirishaji na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, hasa maeneo ya vijijini.”

Pia, anasema serikali imeendelea kuvutia na kutekeleza mikakati ya kuongeza uwekezaji katika vituo vya mafuta vyenye gharama nafuu, hususan vijijini.

KUNAKOONGOZA MATUMIZI 

Anasema, katika mwaka wa fedha 2023/24, mikoa iliyokuwa na matumizi ya juu zaidi ya petroli na dizeli ni, Dar es salaam, Mwanza, Pwani, Arusha na Dodoma, akitaja sababu ni kuwapo shughuli nyingi za kiuchumi na usafirishaji, 

GESI YA ASILIA MAGARI

Anasema katika mwaka 2023/24, serikali ilitekeleza miradi ya kujenga miundombinu ya gesi asilia kwa matumizi ya magari, lengo ni kupunguza gharama za mafuta ya petroli na dizeli, sambamba na kuendeleza matumizi ya nishati safi na nafuu.

Anasema kwa kipindi hicho, vituo vya kujazia gesi asilia (CNG) vitano vilijengwa, vinne viko katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Kuhusu usambazaji gesi asilia, mkurugenzi huyo anasema, katika kipindi hicho usambazaji gesi asilia unapimwa wakati wa kuingia bomba la usambazaji, baada ya kuchakatwa uliongezeka kwa asilimia moja, kutoka futi za ujazo milioni 81,067.16 iliyosambazwa mwaka 2022/23 hadi futi za ujazo milioni 81,868.86.

BITEKO NA TAHADHARI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, anasema wametoka kwenye ukuaji nishati umefikia megawati 1900, kwa kipindi mmoja mahitaji ya umeme nchini yameongezeka kufikia megawati 254.

“Taarifa imetupa tahadhari, imetuonyesha itakapofika mwaka 2035 mahitaji ya umeme nchini yatafika megawati 8855 na itakapofika mwaka 2030, mahitaji ya juu yatafika megawati 4878,” hivyo ndicho anachosema Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Prof. Mark Mwandosya.

Anasema, wataridhika wasiwekeze kwenye nishati kutokana na kasi ya ukuaji uchumi kutahitajika umeme mwingi zaidi.

“Lazima tuanze kujenga vyanzo vingine sasa, miradi ya Luhuji Nyumakali, miradi ya sola ya Kishapu, miradi ya upepo Singida, Makambako.

“Yote hii tuanze kuijenga sasa hivi na tutumie mradi wetu wa Compact tulionao, kama tutapata fedha tuweke ujasiri mkubwa wa kuwekeza kabla hatujarudi hapa kujadili masuala ya mgao.

“Taarifa ya EWURA imetuonyesha hatari ya kule tunapokwenda tujiandae kuikabili hii hatari,”anasema.

Anaongeza: “Upotevu wa umeme umeendelea kuongezeka tumetoka asilimia 14.57 leo tupo 14.61 maana yake ni kwamba lazima tutafute mbinu mbadala ya kuhakikisha upungufu au upotevu wa umeme unaendelea kudhibitiwa, kiwango kinachokubalika kitaalamu ni angalau asilimia 12 sisi tupo juu ya kiwango.”

TANESCO YAAGIZWA

Prof. Mwandosya, anaigiza TANESCO) na mamlaka zingine, kufuatilia mikataba 33 ya uzalishaji na kuuziana umeme, ambayo tangu imetiwa Saini, haijawahi kutekelezwa.

Anaitaja mingi inayotokana na umeme wa sola ambayo miradi 21 ingeweza kuzalisha umeme megawati 157.

“Tufuatilie tujue kuna tatizo gani? lakini je kuna sababu ya kuendelea na mkataba maana mtu mmekubaliana lakini hakuna kinachoendelea ni kama wakati fulani niliwaambia TANESCO wana MoU (makubaliano) nyingi mara hii ya sola, hii ya upepo, MoU ukisaini maana yake umefunga mlango wa mtu mwingine kuingia.

Aidha, anasema katika ripoti hiyo kuna malalamiko 146 yaliyowasilishwa, nyingi yalikuwa kati ya TANESCO na wateja wake, ikilinganishwa na mwaka uliopita yalikuwa 92.

“Kwa mujibu wa taarifa malalamiko mengi waliyoyaona asilimia 27 kuhusu na ankra na asilimia 15 kuhusu uunganishaji, asilimia 12 ni watu waliolalamikia huduma kwa wateja, kile kituo ambacho napenda kukitembelea mara kwa mara asilimia 12 ya malalamiko yanalalamikia jambo hilo,”anasema.

Vilevile anasema asilimia 12 wanalalamikia kuhusu tarrifa, wengine wanadhani bei ni kubwa, asilimia nane wamepata shida kutokana na umeme na asilimia tatu ni uharibifu wa mali.

“Hiki ni kiashiria kingine kuwa EWURA ni kioo cha kutuonyesha wapi kuna matatizo, na tunatakiwa kusimamia kwa karibu sana tuangalie wingi wa malalamiko yanatokea wapi na kama kuna mengine ya kutoa elimu, twendeni kwa wananchi wajue sababu gani imetokea,”anasema.

PENYE MSISITIZO 

Prof. Mwandosya, anasema miradi mikubwa hasa ya umeme, inachukua miaka mingi, kuanzia upembuzi yakinifu hadi kutekelezwa, hivyo anataka kukamilika kwa Bwawa la Nyerere kiwe kichocheo cha kazi kuanza kwa ajili ya miaka ijayo ya kuimarisha uzalishaji wa umeme.