Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Bara Stephen Wasira amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni chanzo cha amani na utulivu unaoendelea kutamalaki Tanzania na kupata maendeleo ya uchumi.
Amesema kama Tanganyika na Zanzibar zingekuwa nchi mbili tofauti usalama ungekuwa mdogo kutokana na ujirani uliopo lakini pia kila upande ungelazimika kutumia bajeti kubwa kuimarisha vikosi vya ulinzi.
Ameyaeleza hayo akiwa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma wakati akihutubia umma kwenye mkutano ambao umefanyika leo Aprili 26, siku ambayo Tanzania inaadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Tunatimiza miaka 61 tangu tuungane hatuna budi kufurahia matunda ya muungano huu uliosaidia kuleta amani na utulivu lakini hata kupata maendeleo ya kiuchumi tofauti na wakoloni walivyotutawala walitumia miaka 75 kujinufaisha wao," amesema nakuongeza:
"Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni ishara watu tuko pamoja na historia ya uhusiano wake ni ya muda mrefu. Ukienda Tanganyika na Zanzibar huwezi kuona utofauti watu ni walewale juzi nilimchukua Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, kutoka Zanzibar kwenda naye mkoa wa Kagera Sophia Mziray nilishangaa nikamuuliza mbona kama ni Mpare wewe akanijibu ni kweli lakini yeye ni Mzanzibar," amesema Wasira.
Kwa mujibu wa Wasira sio hiyo pekee kuna Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake CCM, Taifa, Suzan Kunambi kiasili ni watu wa Morogoro lakini alipomuuliza alimjibu kuwa yeye ni Mzanzibar.
"Ni vigumu kutenga Zanzibar na Tanzania Bara kwa sababu watu wengi walioko Zanzibar wanaasili ya Bara na kile ni Kisiwa watu hawawezi kuchipuka lazima watoke mahali na tukifuatilia historia ya Ukoloni watumwa wote walikuwa wanatoka Bara kwenda kufanya kazi Zanzibar," amesema Wasira.
Amesema kilichotokea ni kutenganishwa tu mipaka na wakoloni lakini jambo la kushangaza kwa sasa viongozi wakija na sera za kuwaunganisha kuwa kitu kimoja baadhi wanajitokeza kubeza, huku akionyesha kushangazwa na hali hiyo.
"Sisi miaka yote tulikuwa wamoja wakoloni wakatugawa tu, na mjue watu ni walewale hakuna kilichobadilika na kuungana kwetu ni chanzo cha Muungano tunaoadhimisha leo 'jana'," amesema Wasira.
Amesema wazungu walikuwa wanagawana Bara la Afrika kama mashamba na wakati huo Tanganyika ilikuwa inaitwa Ujerumani ya Mashariki na kama isingepigwa vita vyapili vya dunia na Uingereza jina lisingebadilika.
"Wazungu sahizi wakiona tunataka kuungana ili tuwe kitu kimoja hawataki wanajua tuna raslimali inaweza kufikia mahali tutawagomea wataenda wapi? na ustaharabu wao umejengwa na utajiri wa Afrika," amesema Wasira.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED