NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2025 watanzania waishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana na kuwa wamoja kwa kuchagua viongozi wanaoweza kuwasilisha ajenda zao kwa wananchi.
Amewataka watanzania kuishi kwa upendo na kushirikiana kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla.
Amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano, akihimiza kukumbukwa kuwa kuwa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume, waliunganisha Tanganyika na Zanzibar katika misingi ya umoja, amani, kuheshimiana.
Biteko amesema hayo Aprili 26, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Soko la Kilombero, wilaya ya Arusha Mjini, mkoani Arusha.
“Sisi tuliopo leo tutakumbukwa kwa lipi, iwe changamoto tunapokumbuka miaka 61 ya Muungano tujue ni alama gani tutaacha kwa watoto wetu,” amesema Dk. Biteko.
Amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2025 watanzania waishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana na kuwa wamoja kwa kuchagua viongozi wanaoweza kuwasilisha ajenda zao kwa wananchi.
“Hicho ndicho kiwe kipimo na viongozi tusitumie tofauti zetu kutafuta kura, usiende kanisani au msikitini kwako kutumia uhalali watofauti zetu kutafuta kura asitokee yeyote kufanya hivyo tuuenzi Muungano na Rais Samia ameapa kuulinda Muungano huu kwa wivu mkubwa,” amesema Dk. Biteko.
Biteko amebainisha kuwa watanzania wasiruhusu taifa kugawanyika kwa sababu yoyote ile, wakumbuke kuwa kama hakuna amani hakuna biashara wala maendeleo yanayoweza kufanyika.
Akiwasilisha salamu za Muungano, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mratibu wa Muungano, Tumsifu Mwasamale, amesema kuwa kwa mwaka huu, ilielekezwa sherehe hizo zifanyike kwa wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED