Shinyanga waadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa usafi wa mazingira kupanda miti

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 05:52 PM Apr 26 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akipanda mti kwenye maadhimisho ya miaka 61 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar mkoani humo
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akipanda mti kwenye maadhimisho ya miaka 61 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar mkoani humo

SERIKALI mkoani Shinyanga imeadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa kufanya usafi wa mazingira pamoja na kupanda miti katika Manispaa ya Shinyanga.

Maadhimisho hayo yamefanyika leo, Aprili 26, 2025, yakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, ambaye amewataka wananchi waendelee kuuenzi Muungano huo kwa kudumisha amani na mshikamano.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Macha amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, umewaunganisha Watanzania kuwa wamoja, kuishi kwa kupendana na kudumisha amani na utulivu wa nchi, hivyo ni vyema ukaendelea kudumishwa.

"Tunapoadhimisha miaka 61 ya muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar, ambao ulituunganisha kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawaomba wananchi tuendelee kuutunza na kuuenzi muungano wetu," amesema Macha.

2

 Aidha, amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hussein Mwinyi, kwa juhudi zao za kuendeleza Muungano.

 Katika hatua nyingine Macha, amekionya chama kimoja cha kisiasa, ambacho kinataka kufanya maandamano mkoani humo yenye vichocheo vya kuvuruga amani, na kwamba wao kama viongozi hawatokubali kuona amani ya mkoa huo ikitaka kuharibiwa.


 “Mkoa huu uko shwari na vyama vyote vimetulia vikijiandaa kushiriki uchaguzi mkuu,lakini kuna chama kimoja tu kipo kinyume, na tunazo taarifa zao za kutaka kupanga maandamano yenye viashiria vya vurugu,hatutakubali kuona amani ya Mkoa wa Shinyanga ikiharibika,” amesema Macha

 Amesema kuwa Tanzania ni nchi ambayo inadumisha demokrasi na kuruhusu vyama vyote vya siasa kufanya shughuli zao za kichama,lakini siyo kutaka kwenye kinyume na Katiba ya nchi

 Aidha,amewataka wananchi wajiandae na uchaguzi mkuu 2025 sababu utakuwepo kwa mujibu wa Katiba ya nchi, ambayo inasema kila baada ya miaka mitano lazima uchaguzi ufanyike,na kwamba hakuna  ambaye atauzuia sababu ni takwa la kikatiba .

Amewataka pia wananchi, kwamba litakapofika zoezi la uboreshaji wa taarifa kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, kwamba wajitokeze kwa wingi kuboresha taarifa zao ili wapate fursa ya kupiga kura na kuwachagua viongozi ambao wanawataka na kuwaletea maendeleo.

 Macha, amewataka pia wananchi waendee kupata miti katika maeneo yao na taasisi za serikali, pamoja na kufanya usafi wa mazingira. Naye Afisa Mazingira na Maliasili Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Ezra Manjerenga, amesema katika maadhimisho hayo ya miaka 61 ya Muungano mkoani humo, imepandwa jumla ya miti 100.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar inasema”Muungano wetu ni Dhamana,Heshima na Tunu ya Taifa: Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”