Serikali yaondoa zuio la mazao Malawi, Afrika Kusini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:40 PM Apr 26 2025

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

Baada ya siku mbili za utekelezaji wa zuio kwa bidhaa za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi, Serikali ya Tanzania imeliondoa kupisha majadiliano.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alitangaza kuanza utekelezaji wa zuio kwa bidhaa hizo baada ya Aprili 17 kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kueleza ifikapo siku hiyo Serikali ya Tanzania itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka mataifa hayo.

Katika taarifa ya Wizara ya Kilimo ya jana Aprili 25, 2025 iliyosainiwa na Waziri Bashe, imesema zuio hilo limeondolewa kuanzia leo Aprili 26.

Kutokana na zuio lililowekwa, amesema Serikali za Malawi na Afrika Kusini zimewasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Kilimo za Tanzania ili kutafuta suluhisho.

Bashe amesema makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba Serikali ya Malawi itatuma ujumbe wake Mei 2, 2025 utakaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje akiambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo ili kukutana na ujumbe wa Tanzania jijini Dodoma chini ya uratibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania.

Kuhusu Afrika Kusini, amesema majadiliano ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania yanaendelea kwa pamoja na Mamlaka za Afrika Kusini zinazohusiana na afya ya mimea na masoko.

"Kwa misingi hiyo, Wizara ya Kilimo inaondoa mazuio yote yaliyowekwa kwa nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia Aprili 26, 2025 tukiamini majadiliano yanayoendelea yataleta suluhisho," imesema taarifa ya wizara.

Bashe amesema Serikali inawahakikishia wakulima na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kuwa, uhuru wa biashara ya mazao ya kilimo kulingana na matakwa ya afya ya mimea, rasilimali za nchi zilizopo na mahusiano mapana ya kidiplomasia kwa faida ya wote.