MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Sukari, Prof Kenneth Bengesi, amesema Tanzania iko mbioni kuondokana na uhaba wa sukari, kutokana na uwekezaji unaoendelea.
Amesema hayo wakati wa kongamano la wadau wa sukari lililoandaliwa na Jumuiya ya chama cha wataalamu wa Miwa na Sukari nchini (TSSCT) katika chuo cha Sukari cha Taifa, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Aidha, wadau mbalimbali wakiwamo wataalamu wa sasa na wa zamani wa miwa na sukari, menejimenti za viwanda vya sukari, bodi, mfuko wa maendeleo ya sukari, wazalishaji wa teknolojia, vyama vya wakulima na wengine, wameshiriki.
Mkurugenzi mkuu huyo, amesema eneo la sukari imeendelea kuwa na maendeleo makubwa hasa katika kipindi cha awamu ya sita, kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwapo kutatuliwa.
Akasema lengo la serikali sio kujitosheleza kwa sukari peke yake, bali pia kuzalisha ziada itakayouzwa nje ya nchi na kupata uhakika wa fedha za kigeni zitakazotumika kutatua changamoto za kijamii na kujenga miundombinu ya kiuchumi.
“Utulivu uliopo kwa miaka ya karibuni umewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa sukari kutoka tani 295,000 miaka saba, nane iliyopita kufikia tani 460,000 zilizorekodiwa mwaka juzi ikiwa ni kiasi cha juu kabisa kwa karibu mara mbili zaidi ya uzalishaji uliokuwapo.
Amesema kwa sasa pia serikali inatoa ruzuru ya mbolea na kuongeza uzalishaji wa miwa sambamba na kurahisisha upatikanaji wa mitaji, kwa kuongea na mabenki na kuweka mazingira mazuri ya mikopo.
Katibu wa Jumuiya ya Chama cha Wataalamu wa Miwa na Sukari Tanzania (TSSCT), Mwanaidi Jaffery, amepongeza jitihada za seriikali kwenye sekta ya sukari na kusaidia uhimilivu, kuongeza uzalishaji wa miwa na sukari na kuziba uhaba wa sukari.
Rais huyo wa TSSCT akasema wao kama wataalamu wamekuwa wakihusika mashambani na viwandani hivyo wamegundua bado kuna changamoto ya matumizi madogo ya TEHAMA, kwa upande wa wakulima wadogo, kumechangia wakulima kupata tija ndogo.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uendelezaji wa Teknolojia na Ushirikiano wa Kitaaluma kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk. Sophia Kashenge, amesema licha ya changamoto nyingi katika sekta ya sukari, bado sekta hiyo imeendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED