Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro kumuenzi Mkapa

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 04:09 PM Apr 28 2025
Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro kumuenzi Mkapa
Picha: Pilly Kigome
Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro kumuenzi Mkapa

CHUO Kikuu cha Kiislamu Morogoro, kinatarajia kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kwa kumshukuru na kutambua mchango mkubwa uliotolewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa.

Kilele cha maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa Juni 20, 2025 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamesemwa leo April 28, 2025 na Makamu Mkuu wa Chuo cha Kiislamu Morogoro(MUU) pia CAG mstaafu Prof. Mussa Assad, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salam.

Prof. Assad amesema kuwa kwa kutimiza miaka 20 chuo hicho kinatambua mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Benjamin Mkapa kwa kutambua na kuthamini kukuza elimu kwa watoto wa kiislamu nchini ambayo ilikuwa chini na kuwapa majengo waanzishe chuo hicho.

Amesema mwaka 2004 Hayati Benjamin Mkapa akiwa Rais alitembelea mkoa wa Morogoro na kuamuru majengo ya Tanesco yatumike kuanzisha chuo kikuu cha kiislamu kwa kuweza kuwainua watoto wa kiislamu ambao ilionekana kuwa elimu yao iko chini kwakuipeleka jamii katika kiwango cha juu cha elimu.

“Yeye ndie alikuwa chanzo  cha kupatikana na kuanzishwa chuo chetu hivyo tutamkumbuka kwa mazuri na kuinua vijana wetu wa kiislamu kupata elimu ya juu,” amesema.

Aidha amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya chuo hicho mkoani Morogoro yatakuwa na programu nyingi ikiwemo kutoa tuzombalimbali pamoja na dua la kuliombea taifa.

Ametoa utofauti wa chuo hicho na vyuo vingine kuwa chuo hicho kwanza kinazalisha wataalamu, kinatoa ushauri katika jamii na kuipeleka kiwangocha juu cha maadili katka jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Shekhe Mkuu wa Tanzania, Shehe Khamis Ngeruko, amesema suala la elimu kwa kila muislamu ni (faradhi) wajibu na ni haki hivyo ni lazima aliendee kwani hata Mwenyezi Mungu aliwaamrisha waislamu wasome kwa lazima hata kwa viboko.

Amefafanua kutokana na umuhimu huo ni lazima kwa kila muislamu aidha afundishe, kuchangia, kuelekeza na namna yoyote ile ili mradi elimu ipatikane.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Taifa (JUWAKITA) pia aliyekuwa Mbunge wa Morogoro Mjini kipindi hicho amesema akiwa kama shuhuda wakati wanakabidhiwa majengo hayo na Hayati Mkapa akiwa na lengo la kuinua elimu nchini ni jambo la kujivunia na kihistoria kutoka kwa chuo hicho.

Amesema elimu ni muhimu kwa kila mtanzania hivyo watamenzi kwa maono yake kwani hata Mwenyezi Mungu amesema tutafute elimu kwa hali yoyote, ili tuweze kutofautiana na wanyama.