Perseus kuanza ujenzi mgodi wa dhahabu wa Nyanzaga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:08 PM Apr 28 2025
Perseus kuanza ujenzi mgodi wa  dhahabu wa Nyanzaga
Picha: Mpigapicha Wetu
Perseus kuanza ujenzi mgodi wa dhahabu wa Nyanzaga

Kampuni ya Perseus ya Nchini Australia yatoa tangazo rasmi la kuanza ujenzi wa mgodi wa dhahabu wa Nyanzaga uliopo Wilayani Sengerema mkoani Mwanza utakaomilikiwa na Kampuni ya Ubia ya Sotta ambapo Kampuni ya Perseus ina umiliki wa hisa za 84% na Serikali ya Tanzania ina umiliki hisa zisizofifishwa za 16% .

Taarifa hiyo iliyotolewa leo tarehe 28 Aprili, 2025 imeeleza kuwa takribani kiasi cha Shilingi Trilioni 1.4 sawa na Dola za Kimarekani Milioni 523 zitawekezwa kujenga mgodi mkubwa unaotarajiwa kuzalisha dhahabu ya kwanza katika robo ya kwanza ya Mwaka 2027.

“Fedha zote za kujenga mgodi zitafadhiliwa na Perseus kupitia mikopo isiyo na riba, ambayo itapelekwa kwenye mradi wa Nyanzaga moja kwa moja. Na fedha hizo zote zipo kwani Perseus ina salio la pesa taslimu na bullion la dola za Marekani milioni 801 kufikia tarehe 31 Machi 2025” ilifafanua taarifa hiyo.

Kwa kutarajia maamuzi ya mwisho ya kuwekeza (Final Investment Decision - FID) katika mradi huo yangepitishwa na uongozi wa juu wa Kampuni ya Perseus, tayari Perseus imetumia takriban dola za Marekani milioni 27.5 katika kutekeleza shughuli za awali za maandalizi ya uwekezaji.

Shughuli hizo za awali za kujenga mradi wa Nyanzaga zilizokuwa zinaendelea ni pamoja na kama kuanzisha eneo la kufanyia kazi,ujenzi wa kempu pamoja na kutekeleza Mpango wa Utekelezaji wa Uhamisho (RAP) na kujenga makao mapya kwa watu walioathiriwa na mradi.

Kufuatia tangazo hilo Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema taarifa hiyo ni njema kwenye kukuza sekta ya madini na ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu mpendwa Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo imeweka mazingira mazuri yanayoendelea kuvutia uwekezaji mkubwa nchini.

 Kutolewa kwa tangazo hilo na Kampuni ya Perseus kumeleta matumaini makubwa na kukata kiu ya wananchi wa Sengerema ambao wameusubiri mradi huo kwa muda mrefu na sasa ndoto yao inakwenda kutimia kwa kuona mradi mkubwa wa kuzalisha dhahabu unaanza ambao utasaidia upatikanaji wa mapato ya serikali,Ajira kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Sengerema na nchi kwa ujumla.