Mwenyekiti wa Alliance for Democratic Change (ADC), Shabani Itutu, amewapokea wanachama wapya waliokuwa viongozi wa chama cha NCCR-Mageuzi kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika 27 Aprili 2025, katika Makao Makuu ya chama hicho, Itutu amesema chama hicho kinashindana na vyama vingine kwa sera nzuri na kwamba ADC imejikita katika kuimarisha demokrasia na usawa kwa kila mwananchi. Amesisitiza kuwa wanachama wapya watafundishwa Katiba ya chama pamoja na Katiba ya nchi ili wawe wanachama bora, wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Miongoni mwa waliopokelewa ni viongozi waliokuwa na nafasi kubwa ndani ya NCCR-Mageuzi, akiwemo Dk. Saganda Khalid Saganda, aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Shinyanga na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa; Michael Makene, aliyekuwa Katibu wa Wilaya ya Ilemela na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi; pamoja na Michael Leiser, ambaye alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa wa chama hicho. Pia alipokelewa Ramadhani Amrani Mrisho, aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Mwanza, Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama.
Kwa upande wake, Mlezi wa ADC, Hamadi Rashid, alisema kuwa chama hicho kinasimamia haki ya msingi ya kila raia ya kuchagua na kuchaguliwa, na kwamba ADC itaendelea kuimarisha demokrasia kwa kuwalea wanachama wake kwa misingi ya haki na amani.
Akizungumza kwa niaba ya waliopokelewa, Dk. Saganda Khalid Saganda alisema kuwa ameamua kujiunga na ADC kutokana na utaratibu wake mzuri wa kuendesha siasa safi inayozingatia haki na usawa. Michael Leiser naye alieleza kuwa alihama NCCR-Mageuzi baada ya kuona chama hicho hakina tena dira ya siasa safi, akisisitiza kuwa ADC ni chama kinachojali maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Michael Makene na Ramadhani Amrani Mrisho pia walitoa pongezi kwa ADC kwa kuweka mazingira bora ya kisiasa yanayowezesha ustawi wa viongozi na wanachama kwa ujumla.
ADC ilitoa wito kwa vyama vyote vya siasa nchini kuhakikisha vinaendeleza amani na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, kwa kuwa amani ni nguzo muhimu kwa maendeleo na ustawi wa demokrasia nchini Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED