Walimu wajazwa 'noti' DED Hai akitoa motisha

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:44 PM Apr 28 2025
Walimu wajazwa 'noti' DED Hai akitoa motisha.
Picha: Mpigapicha Wetu
Walimu wajazwa 'noti' DED Hai akitoa motisha.

Halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, imeanza kutoa motisha kwa walimu wake, kwa kununua kwa Sh. 10,000 kila somo ambalo mwalimu ametoa mwanafunzi au wanafunzi wenye alama 'A' katika mitihani ya kitaifa kwa shule za sekondari.

Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Sekondari katika Halmashauri hiyo, Hellen Mselem, amesema wamefikia uamuzi huo, kwa kuwa rasilimali fedha ni zawadi nzuri, na ni kichocheo kizuri cha kumfanya mwalimu aonekane amethaminiwa wilayani humo.

Alikuwa akizungumza jana katika hafla maalum ya kuwapongeza walimu na wanafunzi wa shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.


"Lengo la kutoa zawadi za motisha ni kuangalia jinsi gani wanafunzi wamefanya vizuri katika matokeo ya kumaliza kidato cha sita, kidato cha nne pamoja na wanafunzi waliofanya upimaji wa mtihani wa utamirifu wa kidato cha pili.


"Tunaangalia na kuthamini ni jinsi gani mwalimu amejitahidi sana kuwezesha matokeo kuwa mazuri. Anajisikia faraja amethaminiwa katika kazi yake. Tunaamini kwamba motisha hii itawajengea walimu hamasa na kuendelea kufanya vizuri zaidi.


...Kwa hiyo, walimu waliopata A katika masomo yao kwa kila somo moja, sisi Halmashauri kupitia OC (fedha za matumizi mengineyo), Mkurugenzi Mtendaji, ametoa fedha na ameelekeza wapewe shilingi 10,000 kwa kila A moja. Hivyo kama amepata A 10 maana yake anapata sh.100,000."