PAPA Francis ambaye amefariki dunia Jumatatu ya Pasaka, aliacha ujumbe muhimu kwa watanzania kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ujumbe huo umeeleza: “Mheshimiwa Rais, nina heshima kubwa kuwasilisha kwa Mheshimiwa (Rais) ujumbe ufuatao uliotayarishwa na Baba Mtakatifu marehemu, Papa Fransisko, siku chache kabla ya kufariki kwake kwa huzuni, kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Muungano wa Tanzania:
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa heshima ya Siku ya Muungano wa Tanzania, ninatoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa na kwa wananchi wenzako.
“Nikiliweka taifa mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ninaomba kwamba awajalie hekima na upole kwa wingi wote wanaoishi ndani yake.
“FRANSISKO, Kwa salamu za upendo na matakwa mema, ninaitumia fursa hii kurudia kuonyesha hisia zangu za heshima ya dhati,” umeeleza ujumbe huo.
Ujumbe huo, umewasilishwa na Balozi wa Kitume, Angelo Accattino, kutoka Vatican, huko Roma.
Kwa mujibu wa ukurasa wa Rais Samia, mtandaoni amejibu: "Kwa unyenyekevu na shukrani, nimepokea ujumbe wa hayati Papa Francisko kwangu, kwa nchi yetu na kwa Watanzania wote, aliouandika siku chache kabla Mwenyezi Mungu hajamwita kwake, na kumkabidhi Balozi wa Vatican hapa nchini, Askofu Mkuu Angelo Accattino."
"Tuendelee kumwombea kwa Mwenyezi Mungu alale mahali pema."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED