Shule 117 zakabidhiwa mipira ya soka

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 01:02 PM Apr 27 2025
Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa wa Lindi, Joseph Mabeyo (katikati), akipokea misaada wa mipira 585 kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Sports Development Aid Ramson, Ramson Lucas
Picha: Ambrose Wantaigwa
Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa wa Lindi, Joseph Mabeyo (katikati), akipokea misaada wa mipira 585 kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Sports Development Aid Ramson, Ramson Lucas

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Sports Development Aid limetoa msaada wa mipira 585 yenye thamani ya Sh milioni 35, kwa shule za sekondari 117, ili kuinua ubora wa michezo kwa wanafunzi.

Akikabidhi msaada huo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Mkurugenzi wa shirika hilo, Ramson Lucas, amesema wanaendesha miradi ya kuboresha maendeleo ya elimu kupitia michezo mkoani humo.

Amesema ugawaji wa mipira hiyo utaboresha mahudhurio na taaluma mashuleni kwa vijana wa kike na kiume ambapo kila mwaka wamekuwa wakishiriki kusaidia vifaa vya michezo, kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Umoja wa Michezo Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA)

Mbali na ugawaji wa vifaa vya michezo, amesema pia wanaendesha mafunzo ya kukabili unyanyasaji wa kijinsia kwa vijana walioko mashuleni pamoja na kupiga vita mila zilizopigwa marufuku.

Akipokea msaada huo, Katibu Tawala Msaidizi Elimu mkoani humo, Joseph Mabeyo, amesema mipira hiyo itasaidia katika kuwaandaa vijana kisaikolojia na kushiriki masomo wakiwa na afya njema.

"Michezo ni ajira na inasaidia kuimarisha afya ya wanafunzi kushiriki masomo muda wote wakiwa mashuleni na hivyo kuinua taaluma katika shule za mkoa wa Lindi,” amesema.

Amesema mkoa huo una shule mbili za amali za sekondari za Mahiwa na Nkoe, walimu wa michezo wameelekezwa kusimamia maandalizi ya wanafunzi watakaoshiriki mashindano ya shule za sekondari yajayo.

Shirika hilo linashughulika na miradi ya maendeleo ya elimu kupitia michezo mkoani humo, kwa kugawa vifaa vya michezo bure katika shule za msingi na sekondari kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita.