Wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 61 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman amesema ipo haja ya kufanyika kwa mabadikiko mkubwa ya mfumo wa Muungano ili nchi zote mbili za washirika zipate haki sawa.
Othman ameyasema hayo leo April 26 katika ukumbi wa Samael Chakechake Pemba alipokua akizungumza na maelfu ya vijana wa chama hicho katika kongamano maalumu la maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano.
Alisema uwepo wa Muungano huu kwa muda mrefu unaikandamiza Zanzibar licha ya kuwa na rasilimali zake nyingi inashindwa kupata maendeleo na kukuza uchumi kama nchi huru.
Alisema pamoja na uwepo wa kasoro nyingi za Muungo na kulalamikiwa, watawala wanashindwa kujali na wamekua wakiongeza mambo mengine mapya kujinufaisha na familia zao.
"Tulianza kulalamika mambo 11 ya Muungano hapo awali lakini sasa tunalalamikia mambo 41 bila wenzetu kujali lolote huku mambo yote hayo yakinufaisha upande wa pili wa Tanzania Bara" alisema.
Aidha Othman ambae pia ni Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar amesema kwa nyakati tofauti viongozi mbali mbali wamekua wakifanya jitihada kumaliza, changamoto hizo lakini hakuna mafanikio ambayo yanapatikana kwa sababu wenye nguvu ndio wenye maslahi.
"Zimeundwa zaidi ya kamati 10 kushughulikia kero za Muungano lakini zote zimeishia njiani na hakuna kilichotimia hadi leo na ndio maana tunasema wenzetu hawana ukweli" alisema.
Sambamba na hilo alisisitiza changamoto hizo zinaiathiri zaidi Zanzibar ikiwemo kukosa mamlaka ya kukopa nje ya nchi fedha ambazo zingeweza kuendesha miradi na kukuza uchumi wa Zanzibar.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED