Dk. Mpango: Njia ya kumuenzi Papa Francis ni kudumisha amani, kujali masikini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:44 PM Apr 26 2025
Dk. Mpango: Njia ya kumuenzi Papa Francis ni kudumisha amani, kujali masikini
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk. Mpango: Njia ya kumuenzi Papa Francis ni kudumisha amani, kujali masikini

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, amesema njia bora ya kumuenzi hayati Papa Francis, aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, ni kudumisha amani na kuwajali masikini.

Dk. Mpango ametoa kauli hiyo mara baada ya Misa ya Mazishi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro – Vatican. Alimsifu Papa Francisco kwa juhudi zake za kutafuta amani duniani, akitaja tukio la kumbusu miguu viongozi wa Sudan kama mfano wa unyenyekevu na msisitizo wa amani.

Aidha, Makamu wa Rais amesema moja ya nyaraka za mwisho zilizotiwa saini na hayati Papa Francis ni barua aliyomwandikia Rais wa Tanzania akimtakia heri ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Katika Misa hiyo, Dk. Mpango aliambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, na Balozi wa Tanzania Vatican, Hassan Mwamweta.

Misa hiyo ilihudhuriwa na watu zaidi ya 400,000, wakiwemo viongozi wakuu kutoka mataifa mbalimbali. Maziko ya Papa Francis yamefanyika katika Basilika ya Santa Maria Maggiore, leo Aprili 26, 2025.