Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kipo katika hatari ya kufutiwa usajili iwapo kitaendelea na kuwatambua viongozi waliovuliwa uongozi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Katika barua ya Msajili iliyotoa taarifa kwa ofisi hiyo imeeleza kuwa inayo mamlaka ya kukifutia usajili chama hicho endapo kitaendelea kuwatambua viongozi hao. “Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inapenda kuwakumbusha wanachama na viongozi wa CHADEMA kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa Msajili anayo mamlaka ya kusimamisha usajili wa chama hicho” imesema sehemu ya barua ya Msajili.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imeendelea na msisitizo wake wa kutoitambua Sekretarieti ya uongozi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inayomjumuisha Katibu Mkuu wake John Mnyika. Sekretarieti hiyo ya CHADEMA iliteuliwa Januari 22 mwaka huu kwenye Baraza Kuu la chama hicho baada ya kupatikana kwa uongozi mpya unaoongozwa na Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED