UMOJA wa Nchi za Denmark, Finland, Norway na Sweden (Nordic) hapa nchini umesema Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuwawezesha vijana wakiwemo wasomi kujiajiri kupitia sekta mbalimbali zikiwemo ya kilimo na mifugo hatua inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa vijana wa Kitanzania.
Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Jesper Kammersgaard,alisema kwa niaba ya mabalozi wenzake walipotembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) pamoja na SUGECO (The Sokoine University Graduate Entrepreneurs Cooperative (SUGECO)ambao unasaidia vijana kuendeleza ujuzi hasa katika nyanja ya kilimo na mifugo.
Mabalozi wa Nordic ,hapa nchini walifanya ziara ya siku moja mkoani Morogoro ili kuona miradi na shughuli mbalimbali zinazofadhiliwa ikiwa ni kuadhimisha maadhimisho ya wiki moja ya ushirikiano baina ya nchi hizo na Serikali ya Tanzania ambayo yaliyoanza Mei 26, 2025 Jijiji Dodoma na kufikia tamati Mei 29, 2025 Jijini Dar es Salaam .
“ Nimefurahi kushwa na SUA hasa SUGECO ambao wanafadhiliwa na Denmark kwa zaidi ya miaka kumi sasa , kwa ujumla wetu tumefurahi namna wanavyo hamasisha kukuza sekta ya kilimo na ufugaji ambapo njia hii inasaidia kuongeza kuwango cha uzalishaji wenye tija katika kilimo na mazao ya mifugo nchini Tanzania “ alisema Balozi Jesper.
Balozi wa Denmark alisema katika kusaidia sekta hiyo hivi sasa wanafunzi zaidi ya 20 wamepatiwa ufadhili wa kufanya kazi za vitendo katika nchi za Nordic zikiwemo na Dernmark na Sweden .
“ Mwanafunzi hawa wanafanya ujuzi zaidi katika nchi hizo na watakaporejea Tanzania wanatumia ujuzi walioupata katika nyanja ya sekta ya kilimo na ufugaji wa kisasa watakuwa na mchango mkubwa kusaidia maendeleo ya nchi yao kuendeleza sekta ya kilimo” alisema Balozi Jesper.
Akizungumza na uongozi wa Chuo Kikuu SUA kwa niaba ya mabalozi wenzake alisema ushirikiano uliopo wan chi za Nordic na Chuo Kikuu hicho umeleta maendeleo ya kisasa kutoka kwenye Ndaki ya Mifugo , Ndaki ya Misitu pamoja Ushirika wa SUGECO ambao unasaidia vijana kuendeleza ujuzi hasa katika nyanja ya kilimo na mifugo.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Profesa Raphael Chibunda alisema uhusiano wa Nchi za Nordic hasa nchi ya Norway ulianza mwaka 1973 wakati Serikali ilipofanya uamuzi wa kuanzisha ufundishaji wa taaluma ya misitu nchini na ndiyo walikuwa watu wa kwanza waliosaidia kuanzisha shahada ya kufundisha masuala ya misitu.
Alisema kwa upande wa Denmark ndiyo walikuwa wa kwanza kusaidia nchi kwenye ujenzi wa Ndaki yao ya Tiba za Wanyama(Vetinary Medicine) na waliendelea kusaidia kwa kipindi cha mwanzo kwa kuleta walimu kuja kufundisha wanafunzi wao.
‘‘Kwahiyo tumewashukuru kwamba kwa kipindi chote hicho wamesaidia chuo chetu kimekua sasa na sisi tumesimama kwa miguu yetu wenyewe na walimu wetu wenyewe na tumeweza kukipanua hiki chuo kwa sababu, ukiangalia hiyo miaka wanatusaidia kilikuwa ni chuo kidogo kilichokuwa na wanafunzi wasiozidi 2,000’’ alisema Profesa Chibunda.
‘‘Tumefuraishwa na Chuo chetu kina wanafunzi zaidi ya 18,000 tumekipanua kwenda kukipeleka nje ya Morogoro ,tuna kampasi mpya katika Mkoa wa Katavi ambayo ni Kampasi ya Mizengo pinda, tuna mashamba ya misitu sehemu mbalimbali nchini kwa hiyo ujio wao ni kuja kuona hayo waliyoyafanya tunayaendelezaje’’ alisema Profesa Chibunda.
Profesa Chibunda alisema wamezungumza kuhusu kuimarisha uhusiano huo na kwenda nafasi kubwa zaidi ikiwemo kuwa na uwezo wa kubadilishana wanafunzi na walimu ambapo walimu wao ni wabobezi na waandamizi waje kufundisha kwa muda mfupi ili wanafunzi wa Chuo chetu waweze kupata nafasi ya kuvuna kutokana na uzoefu mkubwa walionao.
Naye Mkurugenzi wa SUGECO, Revocatus Kimario, alisema ushirikiano na nchi za Nordic umekuwa wa manufaa makubwa, kwani zaidi ya vijana 850 wamepelekwa nje ya nchi hizo kwa mafunzo na uzoefu wa kilimo cha kisasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, na kati ya hao, vijana 535 walipelekwa mwaka 2023.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED