Wafanyabiashara mbalimbali mkoani Morogoro wamesema wanatarajia Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 itakayowasilishwa Bungeni kesho iwe na majibu ya changamoto zao, zikiwemo maboresho ya huduma za maji na nyongeza ya fedha za ndani zitakazosaidia kupunguza makato ya ushuru mbalimbali yanayowaumiza.
Wakizungumza leo Juni 11, 2025, wakazi hao wamesema licha ya bajeti zilizopita kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maji, bado changamoto ya uhaba wa huduma hiyo ni kubwa, hasa katika maeneo ya Manispaa ya Morogoro.
Zacharia Uvuvwe, mkazi wa Manispaa ya Morogoro, amesema anatarajia bajeti ya mwaka huu iwe na mipango thabiti itakayohakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika ya maji.
“Kwa muda mrefu tumesikia bajeti zikielekeza fedha kwenye miradi ya maji, lakini hali halisi bado ni ile ile. Tunapata maji kwa mgao, jambo ambalo linaumiza wananchi,” amesema Uvuvwe.
Kwa upande wake, Happy Mganga, mfanyabiashara wa matunda katika soko la Faya, amesema wanaendelea kukabiliwa na mzigo mkubwa wa ushuru wanapofanya biashara zao. Amesema wanalipa ushuru wa Sh1,000 mara wanaponunua bidhaa kwa kila tenga moja sokoni, ushuru ambao huitwa wa usafi, kisha wanapofika sokoni kwao hulazimika tena kulipa ushuru mwingine kwa mzigo huo huo.
“Ukiweka na gharama ya usafiri wa shilingi 7,000 kwa gari moja la mizigo, unaweza kununua papai kwa Sh500 lakini hadi lifike sokoni linakuwa limegharimu Sh1,000. Hali hii inatufanya tupate hasara au faida ndogo sana, huku tukikumbwa na changamoto nyingine kama kodi za nyumba, gharama za shule kwa watoto na chakula cha familia,” amesema Mganga.
Wamesema matarajio yao makubwa ni kuona bajeti mpya ikiweka mpango wa kupunguza mzigo wa ushuru usio na tija kwa wafanyabiashara wadogo, pamoja na kuhakikisha huduma za msingi kama maji zinapatikana kwa uhakika.
Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 inatarajiwa kusomwa kesho Bungeni mjini Dodoma, ikiwa na matarajio ya kugusa maeneo mbalimbali muhimu kwa maendeleo ya taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED