Baadhi ya wabunge na wadau wa sekta ya fedha wamepongeza Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026, wakisema imeleta nafuu kwa wananchi na kuweka mazingira bora kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mbunge wa Viti Maalum, Ritta Kabati, amesema bajeti hiyo imeleta afueni kwa wananchi kwa kupunguza utitiri wa kodi zilizokuwa kero kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Pia amepongeza hatua ya Serikali kuweka usimamizi maalum kwa wafanyabiashara wa kigeni ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilalamikiwa na wafanyabiashara wa ndani.
“Tumeona kuna sheria itakayorekebishwa ili wafanyabiashara wa ndani wapewe kipaumbele. Pia tumeona miradi mingi ya maendeleo imezingatiwa, ikiwamo ya umwagiliaji ambayo sasa imetengewa fedha nyingi. Kilimo sasa hakitakuwa cha kubahatisha kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima waliokuwa wakilima bila uhakika. Pia ruzuku kwenye mbolea itaendelea,” amesema Ritta Kabati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Akiba, Silvest Arumasi, alisema bajeti hiyo inaakisi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mageuzi jumuishi yanayowahusisha wananchi wote.
Amesema bajeti hiyo imelenga maeneo mawili muhimu: kuendeleza miradi ya kimkakati inayochochea uchumi na kuboresha mazingira ya sekta binafsi kushiriki katika ukuaji wa uchumi.
“Tunaona Serikali inaendelea kutengeneza mifumo ya kujitegemea. Kuna maeneo ya kodi na sheria yameguswa, ikiwamo suala la biashara. Waziri amesema mamlaka zisitumie kufunga biashara kama suluhisho la changamoto za wafanyabiashara bali watumie njia mbadala. Hii itasaidia taasisi za kifedha kutoathirika pale biashara zinapofungwa kwa watu waliokopa mitaji,” amesema Arumasi.
Aidha, amesema bajeti hiyo imetoa nafuu kwa wananchi kwa kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye miamala ya kielektroniki kutoka asilimia 18 hadi asilimia 16, hatua itakayochochea matumizi ya huduma za kifedha na kupunguza matumizi ya fedha taslimu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Shukurani Manya, amesema bajeti hiyo itaendeleza utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ukiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na vipande vilivyobaki kuelekea Mwanza na Kigoma.
Ameongeza kuwa bajeti hiyo pia imeendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuongeza tija katika kilimo, huku akisisitiza kuwa Tanzania iko katika mwelekeo mzuri wa maendeleo, ikizingatiwa pia uboreshaji unaoendelea katika sekta za afya na elimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED