Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/26 serikali imependekeza asilimia 70 ya ushuru wa vilevi, mafuta, michezo ya kubeti na magari kutoka nje kugharamia mpango wa kudhibiti maambukizi ya Ukimwi na Bima ya Afya kwa Wote.
Akiwasilisha Makadirio ya Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni leo Juni 12,2025, amesema hatua hiyo inakuja kutokana na mabadiliko ya kisera yanayoendelea duniani yamesababisha wadau muhimu wa maendeleo kupunguza misaada iliyokuwa inatolewa kwa ajili ya huduma za afya ikiwemo kukabiliana na kudhibiti magonjwa mbalimbali hususan UKIMWI.
“Serikali inapendekeza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato ili kupunguza nakisi ya kibajeti iliyotokana na kupungua kwa misaada hiyo kwa kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali,”amesema.
Aidha,amesema serikali inapendekezwa asilimia 70 ya mapato yatakayoongezeka ipelekwe kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) na asilimia 30 ipelekwe kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.
Waziri Mwigulu amesema anapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kilevi vinavyozalishwa na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi kwa Sh. 20 kwa lita kwa bia.
Sh. 30 kwa lita kwa mvinyo unaotambulika na Sh. 22.06; Sh. 50 kwa lita kwa pombe kali na vinywaji vingine.
Aidha, amesema inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 ili kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielektroniki kutoka asilimia 17 hadi asilimia 17.5.
Pia, kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, SURA 220, ili kutoza kiasi cha Sh. 10 kwa kila lita ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa.
Aidha, amesema inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, SURA 123 ili kutoza kiwango cha asilimia 0.1 kwenye thamani ya soko ya madini;
Pia, kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, SURA 41 ili kuongeza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi (Winning tax) kwenye michezo ya kubashiri matokeo (sports betting) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15; na kwenye michezo ya kasino ya ardhini (land based casino) kutoka asilimia 12 hadi asilimia 15.
Amesema kutoza magari na mashine (heavy machines) zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kama Sh. 50,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kati ya 0 -1000; Sh. 100,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kuanzia 1001-1500; Sh. 150,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kuanzia 1501-2500; Sh. 200,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kuanzia 2501 na zaidi; Sh.250,000 kwa mashine (Excavators, Bulldozers, Fork Lifts).
Amesema kutoza Sh.500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya treni; na kutoza Sh.1,000 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya anga.
“Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh. milioni 586,404.9.”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED