Wadau washauri mambo manne kumaliza ukatili wa kijinsia

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 09:58 PM Jun 12 2025
Wadau washauri mambo manne kumaliza  ukatili wa kijinsia
Picha:Mpigapicha Wetu
Wadau washauri mambo manne kumaliza ukatili wa kijinsia

Mkutano wa wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono umeazimia hatua nne muhimu zitakazosaidia kukomesha vitendo hivyo nchini, ikiwemo utoaji wa elimu mtaa kwa mtaa ili kufikisha ujumbe kwa jamii nzima.

Maazimio mengine yaliyofikiwa ni pamoja na kushirikisha Kampeni ya Safari Salama kwa Wanafunzi na Wasichana inayoratibiwa na Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI) kwa ufadhili wa Women Fund Tanzania Trust (WFT-T), katika ngazi zote za mikutano ya jamii, mabaraza ya watoto, na vikundi vya wanawake na vijana.

Aidha, wadau wamependekeza kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ili rushwa ya ngono isitafsiriwe tu kwa watu wenye mamlaka kazini kama sheria ilivyo sasa, bali iwe ni kwa watu wengine wenye ushawishi mkubwa katika maisha ya kila siku, kama vile makondakta wa magari na waendesha bodaboda.

Pia iliazimwa kuhamasisha uanzishwaji na uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi na sekondari ili kuwajengea wanafunzi ujasiri wa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ya ngono na ukatili, sambamba na kuanzisha klabu za watoto mitaani ili kuwafikia wale ambao hawapo shuleni.

Maazimio hayo yalitolewa Juni 10, 2025 jijini Dar es Salaam, kufuatia majadiliano ya pamoja kati ya maofisa kutoka Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, na wadau kutoka WAJIKI.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma kutoka TAKUKURU Kinondoni, Dorothea Mrema, alisema changamoto kubwa inayokwamisha upatikanaji wa haki katika kesi za ukatili wa kijinsia ni tabia ya wahusika kukubaliana kimya kimya, kinyume na sheria.

“Watu wengine wanaona aibu kuzungumzia masuala ya kingono. Wahanga wanakosa ujasiri wa kutoa taarifa. Ni muhimu tujenge ujasiri wa kutoa taarifa pale mtu anapofanyiwa ukatili,” alisema Mrema.

Aliongeza kuwa kukosekana kwa utashi na weledi kwa baadhi ya taasisi zinazoshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono pia kunachangia baadhi ya wahanga kukosa haki.

“Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake ili kufanikisha mashauri ya ukatili wa kijinsia. Hili si jambo la kupuuzia, kwani linaweza kumkuta yeyote,” alisisitiza.

Aliwahimiza wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ya ngono kupitia namba 113 bure, inayopatikana masaa 24 kila siku.

Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu wa Kata ya Bunju, Lilian Chillo, alisema kupitia kampeni za WAJIKI wamepata mwanga mkubwa kuhusu namna ya kuzuia ukatili huo, na kwamba mpango wao wa sasa ni kuzifikia shule zote za serikali na binafsi ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi na walimu.

“Nia yetu ni kuhakikisha kampeni hizi zinawafikia watu wengi zaidi. Tunapojielekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, tuna kaulimbiu isemayo ‘Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tunapokwenda,’ kaulimbiu ambayo inatufikirisha kama wadau juu ya wajibu wetu katika kuhakikisha watoto wanaishi kwenye mazingira salama,” alisema Chillo.

Awali, akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza, alisema anaamini utekelezaji wa maazimio hayo utaongeza kasi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini.

“Nimeamua kuwakutanisha wadau hawa ili tuweke mikakati ya pamoja kuimarisha kampeni yetu ya Safari Salama kwa Wanafunzi na Wasichana Bila Rushwa ya Ngono na Ukatili Inawezekana, na tunaamini matokeo yake yatakuwa chanya zaidi,” alisema Mawinza.