Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua rasmi Kituo cha Mawasiliano chenye lengo la kuimarisha mawasiliano na kuwahudumia kwa ufanisi wadau mbalimbali wa sekta ya elimu nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, Naibu Waziri wa Elimu, Omar Kipanga, amesema kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho kunakuja katika kipindi muafaka ambapo Wizara inatekeleza Sera mpya ya Elimu na Mafunzo pamoja na mitaala iliyoboreshwa.
Amesisitiza kuwa kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa katika kutoa taarifa sahihi, ufafanuzi wa sera, na kushughulikia hoja za wananchi kuhusu elimu.
“Mageuzi yoyote ya kielimu yanahitaji kueleweka vizuri na kukubalika na jamii. Kituo hiki kitakuwa kitovu cha mawasiliano kati ya Wizara na walimu, wanafunzi, wazazi pamoja na wadau wengine wa elimu,” amesema Kipanga.
Kituo hicho kimeboreshwa kwa usaidizi wa Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola (FCDO), chini ya Mpango wa Shule Bora.
Mpango huo una thamani ya pauni milioni 89 (sawa na takriban Shilingi bilioni 271 za Kitanzania) na unalenga kuboresha ubora wa elimu, ujumuishi, na usalama wa mazingira ya kujifunzia kwa wasichana na wavulana kwa kipindi cha miaka sita.
Kupitia kituo hicho, Wizara itakuwa na uwezo wa kujibu haraka hoja na malalamiko ya walimu, wazazi na wanafunzi;kusambaza taarifa muhimu kuhusu sera, mitaala na miongozo ya elimu; Kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara na jamii na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa mipango ya elimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED