BAJETI KUU YA SEIKALI: Wachambuzi wasema mwaka wa neema, wataka ajira kwa vijana

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 03:12 PM Jun 12 2025
Bungeni.
Picha: Mtandao
Bungeni.

Wakati Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26 ikisubiriwa leo, wananchi na wachambuzi wa masuala ya fedha na uchumi wameeleza matarajio yao, wakitaka hatua zaidi zichukuliwe kupunguza gharama za maisha na kuongeza fursa zaidi za ajira, hasa kwa vijana.

Bajeti hiyo itakasomwa kesho na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, ikibeba matarajio makubwa kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwamo wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na watunga sera.

Machi 11, 2025, Dk. Mwigulu, akiwasilisha mapendekezo ya serikali ya bajeti ya 2025/26, alisema wanatarajiwa kukusanya na kutumia Sh. trilioni 57.04 ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.4 kutoka Sh. trilioni 50.3 za mwaka 2024/25.

Katika bajeti hiyo, maeneo sita mahususi yatapewa kipaumbele ambayo ni ugharamiaji Deni la Serikali, mishahara, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na uimarishaji demokrasia  nchini, kuimarisha, amani, utulivu na usalama na maandalizi ya fainali za AFCON 2027.

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara, Kilimo na Viwanda Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Dodoma, Ringo Iringo, alisema wanatarajia bajeti ya mwaka ujao itakwenda kujibu changamoto zinazowakabili wazalishaji bidhaa mbalimbali wa ndani, ukiwamo utitiri wa kodi kwa wazalishaji.

"Tunatarajia bajeti ijayo iwe na majibu ya mzigo wa kodi kwa wazalishaji bidhaa mbalimbali wa ndani, ipunguze pia mzigo wa kodi lakini iongeze wigo wa ukusanyaji mapato ya ndani," alisema Iringo.

Alisema kuwa pia watarajia kuona bajeti ambayo inakwenda kufanya uwekezaji mkubwa kwenye uboreshaji miundombinu ya uzalishaji bidhaa za ndani pamoja na miundombinu ya kufikisha bidhaa hizo kwa walaji.

"Tunatarajia bajeti hii kufanya uwekezaji mkubwa kwenye kuboresha mazingira ya uchakati na uzalishaji bidhaa za ndani lakini pia miundombinu kwa ajili ya kufikisha bidhaa hizo kwa walaji lakini pia kuboresha upatikanaji umeme wa bei nafuu na wa uhakika ili kuongeza ubora wa bidhaa zetu na zishindane na zile kutoka nje," alisema Iringo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) Taifa, Paul Loisulie, alisema kwa kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi, hawatarajii makubwa kutoka kwenye bajeti kwa kuwa kuna dhana imejengeka kuwa kiasi kikubwa cha bajeti kinakwenda kugharamia uchaguzi.

"Lakini kwa upande mwingine baadhi wanaamini kwamba mwaka wa uchaguzi ndio ahadi nyingi zinatekelezwa. Uchaguzi wa mwaka huu ni wa saba tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.


"Kwa hiyo pamoja na bajeti yetu kuendelea kuwa tegemezi, haitarajiwi mkwamo wowote kwenye upangaji bajeti ya kuendesha nchi kwa ujumla wake.

"Binafsi ninaamini kwamba pamoja na uchaguzi ulioko mbele yetu, serikali itazingatia vipaumbele vya msingi katika bajeti tarajiwa. Pia ninatarajia kuona vyanzo vingine vya mapato tofauti na vile vilivyozoeleka," alisema.


Mkazi wa Bahi, Job Mndolosi alisema kumekuwa na kupanda kwa gharama za maisha, hivyo ni muhimu bajeti ijayo ielekezwe katika kupunguza bei ya bidhaa muhimu kama mafuta, sukari, unga na umeme.


"Gharama za maisha kwa sasa ziko juu. Kuna vitu ambavyo mwananchi wa kawaida anatumia vipo juu sana.


"Hata nyama imepanda mno, tulikuwa tunanunua kati ya Sh. 9,000 na 10,000 kwa kilo lakini kwa sasa ni Sh. 12,000, huyu mwananchi wa kawaida. Kukutana na nyama kwa sasa ni kama dhahabu, ninaamini gharama za maisha zikishuka, itakuwa rahisi bidhaa zingine kupatikana kwa bei nafuu," alisema.


Katika hili, mwananchi huyo alishauri serikali kuondoa au kupunguza baadhi ya tozo na kodi zinazoathiri moja kwa moja maisha ya mwananchi wa kawaida, gharama za uzalishaji kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo ili bidhaa zipatikane kwa bei nafuu.

Mkazi wa Dodoma, Maimuna Mageni alisema zaidi ya nusu ya Watanzania ni vijana na wana matarajio makubwa katika bajeti kuwa italeta ajira na fursa za kujiajiri kwa kuongezwa fedha kwenye mifuko ya uwezeshaji wa vijana na wanawake, maarufu mikoa ya asilimia 10.


"Hata kwenye uboreshaji elimu ya ufundi na ujuzi wa kazi, tunaona mabadiliko ya sera na mitaala ya elimu inayolenga kumfanya mwanafunzi awe na ujuzi stahiki kwenye soko la ajira.


"Ni muhimu kupitia bajeti hii waaangalie hawa wenye ujuzi wanasaidiwaje, hata vitendea kazi, maana wengine ujuzi wanao lakini hawana mitaji wala vitendea kazi. Turahisishiwe upatikanaji mikopo ya riba nafuu kwa vijana ili kuanzisha biashara ndogo ndogo na za kati," alisema.


Mkulima wa Mpunguzi, Gabu Joseph alisema katika sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, wanatamani kuona upatikanaji pembejeo bora kwa bei nafuu, miundombinu ya umwagiliaji, maghala ya kuhifadhi mazao na soko la uhakika kwa wakulima na usimamizi wa bei za mazao.

BAJETI ZA KISEKTA

Bunge limepitia na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2025/26 kwa wizara mbalimbali za kisekta, ambapo kiasi kikubwa cha fedha kimeelekezwa kwenye maeneo ya kimkakati kwa maendeleo ya taifa.

Wizara ya Fedha, kwa mfano, imeidhinishiwa Sh. trilioni 20.3, kipaumbele kikuu ni kugharamia Seni la Serikali linalotarajiwa kuiva ambalo linafikia Sh. trilioni 14.22.
Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ikihusika na masuala ya utawala bora na huduma za jamii, imepata Sh. trilioni 11.78 kutekeleza vipaumbele 14, ukiwamo usimamizi wa mapato na matumizi katika ngazi za serikali za mitaa.

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imepangiwa Sh. trilioni 3.6 kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa kijeshi na kutoa mafunzo ya uzalendo kwa vijana.

Wizara ya Uchukuzi imetengewa Sh. trilioni 2.75, ikilenga uboreshaji reli, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na mkakati maalumu wa reli ya TAZARA.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeidhinishiwa Sh. trilioni 2.44 kutekeleza sera, mitaala na kuboresha elimu ya ufundi. Wizara ya Ujenzi itatumia Sh. trilioni 2.28 kuendeleza barabara na viwanja vya ndege.

Wizara ya Nishati imepangiwa Sh. trilioni 2.246 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hususan umeme vijijini na nishati safi ya kupikia wakati Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeidhinishiwa Sh. trilioni 2.07 kudumisha usalama.

Wizara ya Afya imeidhinishiwa Sh. trilioni 1.62 kwa vipaumbele vya kinga, matibabu na utafiti wa afya wakati Wizara ya Maji imepangiwa Sh. trilioni 1.16 kutekeleza miradi 1,544 ya maji kote nchini.
Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Ikulu imeidhinishiwa Sh. trilioni 1.35 kusimamia ajira, malimbikizo ya mishahara na uhakiki wa taarifa za watumishi. Wizara ya Kilimo imeidhinishiwa Sh. trilioni 1.2 kutekeleza miradi ya umwagiliaji, pembejeo na thamani ya mazao.

Wizara ya Katiba na Sheria imeidhinishiwa Sh. bilioni 687.7 kufanya maboresho ya huduma za kisheria. Ofisi ya Waziri Mkuu imeidhinishiwa Sh. bilioni 595.3, pamoja na Sh. bilioni 186.79 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imepangiwa Sh. bilioni 519.66, huku CHAN 2024 na AFCON 2027 zikiwa sehemu ya vipaumbele vya serikali katika wizara hiyo.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepangiwa Sh. bilioni 476.7 kutekeleza vipaumbele vikuu vinne vya kuongeza uzalishaji, kuboresha masoko, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi na kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta hizo muhimu kwa uchumi wa taifa.

Wizara ya Maliasili na Utalii imeidhinishiwa Sh. bilioni 359.98, ikilenga kutangaza utalii kitaifa na kimataifa, kuendeleza mazao ya kimkakati ya utalii, kuboresha miundombinu ya sekta hiyo na kutumia teknolojia ya kisasa katika uhifadhi na uendeshaji shughuli za utalii.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepangiwa Sh. bilioni 340.5 kuimarisha diplomasia, ushirikiano wa kikanda na kimataifa na kuendeleza uhusiano wa karibu na mataifa washirika.

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imepangiwa Sh. bilioni 291.5 kutekeleza miongozo ya sekta, kuboresha huduma za mawasiliano na posta na kuimarisha biashara mtandao.

Wizara ya Madini imeidhinishiwa Sh. bilioni 224.98 ili kuimarisha ukusanyaji maduhuli, kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa na kuwainua wachimbaji wadogo. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepangiwa Sh. bilioni 164.15 ili kuleta mageuzi katika utoaji huduma za ardhi.

Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) imetengewa Sh. bilioni 148.6 ili kuratibu Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Wizara ya Viwanda na Biashara imepangiwa Sh. bilioni 135.79 ili iendeleze viwanda na miradi ya kimkakati.

Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imeidhinishiwa Sh. bilioni 81.86 ili kuratibu masuala ya Muungano na mazingira, na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imepangiwa Sh. bilioni 76.057 kuimarisha ustawi wa jamii na ushiriki wa wananchi kwenye miradi ya maendeleo.