Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, amesema licha ya takwimu kuonesha kupungua kwa utumikishaji watoto nchini, imepanga kufanya ukaguzi maalum kwa wiki mbili kwenye maeneo mbalimbali ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaotumikisha watoto.
Akizungumza jijini hapa katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Watoto, Katambi amesema takwimu zinaonesha kuwa utumikishaji huo umepungua kutoka asilimia 29 mwaka 2014 hadi asilimia 24.9 mwaka 2021, kwa mujibu wa Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi uliofanywa na Serikali.
Katambi amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha watoto wote nchini wanalelewa katika mazingira salama na huru dhidi ya ajira haramu.
Amesema ukaguzi huo utafanyika kwenye hasa ya migodi, mashamba, viwanda na maeneo mengine yote ambayo kazi zinafanyika.
Hata hivyo, amesema serikali imeanzisha mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mpango Kazi wa Taifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA II, 2024/25–2028/29) na Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto, ambao unalenga kuunganisha nguvu za wadau wote wa maendeleo, mashirika ya kiraia na jamii kwa ujumla.
“Ni marufuku kutumikisha watoto, nitoe wito kwa waajiri wote nchini kuhakikisha hawajihusishi na ajira za watoto. Kaguzi zinaendelea kufanyika na wale watakaobainika, sheria itachukua mkondo wake bila ajizi,” ameonya Katambi.
Naye, Mratibu wa miradi kitaifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Glory Blasio, amepongeza Tanzania kwa hatua kubwa ya kukabiliana na utumikishaji huo huku akidai kwa kiasi kikubwa utumikishaji bado upo kwa watoto wa kike.
Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, amesema katika kuadhimisha siku hiyo watafanya kaguzi na kutoa elimu kwa wazazi kujiepusha na utumikishaji watoto kwa kuwa unakiuka sheria na miongozo ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED