Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba amesema utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/26 unaweza kuathiriwa na vihatarishi vinavyoweza kujitokeza na hivyo kusababisha kutofikiwa kwa shabaha na malengo ya bajeti.
Akiwasilisha makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2025/26 amevitaja viashiria hivyo kuwa ni mabadiliko ya bei za bidhaa muhimu; kuongezeka kwa riba za mikopo; kushuka kwa thamani ya shilingi; madeni sanjari; mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili;
Vingine ni migogoro ya kisiasa, mahusiano ya kidiplomasia na mabadiliko ya sera za washirika wa maendeleo pamoja na udukuzi na shambulio la mifumo ya kielektroniki.
“Endapo vihatarishi hivyo vitatokea vinaweza kusababisha: kutofikiwa kwa lengo la ukusanyaji wa mapato; kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi; kuongezeka kwa gharama za bidhaa, malighafi,
“Huduma na utekelezaji wa miradi; kuongezeka kwa gharama za kuhudumia deni la serikali; na kuongezeka kwa gharama za mikopo ya kibiashara katika masoko ya fedha.
Aidha, athari nyingine ni pamoja na: kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo; kuongezeka kwa nakisi ya bajeti; kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo; uharibifu wa miundombinu; na kuongezeka kwa madai na madeni ya wazabuni na watoa huduma.
Amesema ili kukabiliana na athari za vihatarishi katika utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2025/26, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali .
Ametaja kuwa ni kutekeleza na kusimamia sera za fedha na bajeti; kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kuimarisha Upatikanaji wa Fedha za Kigeni; kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034);
Pia, kuimarisha usalama katika mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa fedha za umma na shughuli za serikali; kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032); na kusimamia utekelezaji wa sheria ya mikopo, misaada na dhamana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED