Serikali imesema kuwa imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki ya kujipatia kipato kupitia ajira, kujiajiri na shughuli za biashara.
Hayo yamesemwa leo Juni 12, 2025, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipokuwa akisoma hotuba ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni jijini Dodoma.
Profesa Mkumbo amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kuondoa baadhi ya gharama za lazima katika kipindi cha miaka minne iliyopita (2021–2024).
Ameeleza kuwa hatua hizo zimesaidia kuwaokolea wananchi kiasi cha shilingi trilioni 5.7, ambapo jumla ya wananchi 11,036,444 wamenufaika moja kwa moja na mpango huo.
“Kwa jitihada hizo, Serikali imefanikiwa kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi, huku ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watu kujiingiza kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi,” amesema Profesa Mkumbo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED