“Wanasema bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi, lakini kwenye biashara bahati inakujaka pale unapo piga hesabu sahihi nakuwekeza jitihada” anasema Laurence Mollel, dereva wa teksi aliyewahi kuwa mfanyakazi wa kawaida kwenye kampuni ya bima, jijini Arusha. Mwaka 2021, Mollel aliacha kazi yake ya ofisini bila mpango madhubuti wa biashara — ila tu alijua moja: kazi ya kukaa nyuma ya dawati haikuwa ikimsaidia kifedha.
“Kazi ilikuwa ya kurudia rudia, muda ulikuwa mgumu, na mshahara haukuwa ukikidhi maisha,” anasema Mollel.
Alichukua uamuzi wa kubadilisha maisha: alinunua gari lililotumika na akajiunga na Indrive. “Nilitaka udhibiti wa muda na kipato changu. Ride-hailing ilinipa nafasi hiyo,” alieleza.
Mwaka mmoja baadaye, maisha yake yalikuwa tofauti. Alinunua gari la pili na kulikodisha kwa dereva mwingine, akiongeza kipato zaidi. Alipoanza kuona magari ya watalii kama Land Cruiser yakikatiza barabara za Arusha, ndoto yake ilichukua mwelekeo mpya. Akaweka akiba na kununua Toyota Alphard, gari linalomruhusu kuwahudumia wateja wa uwanja wa ndege na watalii.
Kuanzishwa kwa Bolt katika soko la Arusha kulimpa nafasi zaidi ya kupata wateja kupitia majukwaa mawili. Kile kilichoanza kama jaribio sasa ni biashara kamili.
Kwa mujibu wa tovuti ya Paylab.com, madereva wa teksi nchini Tanzania hupata kati ya TSh651,000 hadi TSh1.5 milioni kwa mwezi, huku makarani wa ofisini wakipata wastani wa TSh765,000. Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa sekta ya ride-hailing inalipa zaidi pale inapoendeshwa kwa weledi.
Mollel anakumbuka mshahara wake wa mwisho akiwa bima — na sasa, hatua aliyofikia. “Sekta hii imenibadilishia maisha,” anasema huku akirekebisha kioo cha nyuma.
“Sasa sifanyi kazi tu — najenga.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED