Majimbo sita CCM Singida kufa, kupona

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 02:48 PM Jun 11 2025
Majimbo sita CCM Singida kufa, kupona
Picha: Nipashe Digital
Majimbo sita CCM Singida kufa, kupona

Ikiwa imebaki siku 17 zoezi la kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), majimbo sita mkoani hapa yametajwa kuwa ya kufa na kupona baada ya vigogo wengi kutajwa kujitosa kuchuana na wabunge wa sasa.

CCM ilitangaza mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 kuanzia  Juni 28, mwaka huu. 

Majimbo hayo ambayo yanaonekana kuwa na mchuano mkali kutokana na vigogo wengi kutajwa kuingia kwenye kinyang’anyiro kuwakabili wabunge wa sasa ni pamoja na Singida Mjini, Iramba Mashariki, Singida Mashariki na Ilongelo ambalo kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kulibadili lilikuwa likijulikana kama Singida Kaskazini. 

Singida Mjini ambalo mbunge wa sasa ni Mussa Sima, wanachama wengi wa CCM wanatajwa kujipanga kuwania ubunge, akiwemo Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu, Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Singida, Juma Kilimba, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Pamba, Sajjad Haider na Charles Kisuke, mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji madini.

Wengine ni pamoja na Mjumbe wa NEC CCM mstaafu, Hassan Mazala na Mwalimu Hanai, waliowahi kuingia kwenye kinyang’anyiro katika chaguzi zilizopita. 

Katika Jimbo la Ilongero, mbunge wake wa sasa Ramadhani Ighondo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Waziri mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ambaye uchaguzi uliopita aligombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kushindwa, lakini sasa amerejea CCM na kutajwa kuwa atagombea ubunge jimbo hilo. 

Mbunge Ihondo pia anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mfanyabiashara maarufu anayemiliki viwanda vya magodoro, Haider Gulamali ambaye naye ametajwa kuingia ulingoni ikiwa atafanya hivyo, itakuwa ni mara yake ya pili kuingia kwenye kinyang’anyiro na mwingine ni Hery Kundya ambaye ni mwalimu. 

Jimbo la Singida Mashariki ambalo mbunge wake ni Miraji Mtaturu, nalo limetajwa kuwa la moto baada ya Thomas Mgonto, mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam, kutajwa kutaka kuingia katika jimbo hilo. 

Mwingine ni Nusrat Hanje, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida kupitia CHADEMA, ameweka wazi kuwa atagombea katika jimbo hilo kupitia CCM. 

Jimbo la Manyoni linaloongozwa sasa na Dk. Steve Chaya, Katibu Tawala Mkoa wa Singida mstaafu, Doroth Mwaluko anatajawa kulinyemelea na wengine Jamali Kuigwa na mbunge mstaafu wa jimbo hilo, Daniel Mtuka.

Katika Jimbo la Iramba Mashariki, mbunge wake Francis Mtinga, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida kupitia CHADEMA, Jesca Kishoa ambaye ametangaza kujitoa chama hicho na sasa anapiga jalamba kugombea kupitia CCM. 

Wengine wanaotajwa kutaka kuingia katika kinyng’anyiro hicho ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega na kada mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Baraka. 

Jimbo la Itigi linanyemelewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Yohana Msita kumkabili mbunge wa sasa, Yahaya Masare. 

Majimbo ambayo hayana upinzani na wabunge wake wanatajwa hayatakuwa na upinzani ni Jimbo la Iramba Magharibi ambalo mbunge wake ni Dk. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Fedha, Jimbo la Singida Magharibi linaloongozwa na mbunge Elibariki Kingu.