Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita imemhukumu Ramadhani Katoro (25) Dereva wa Bajaji kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kubaka msichana mwenye umri wa miaka 17 ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwatulole baada ya kumtorosha binti huyo na kumuweka kinyumba kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Bruno F. Bongole baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipokuacha shaka yoyote.
Hakimu Bongole alisema Mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na wanaume wengine wenye tabia za kuwabaka watoto wa shule kama yake.
Alisema upande wa mashtaka ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa serikali Concessa Desideri ambaye alipeleka hapo mahakamani mashahidi 6 na kielelezo kimoja ambavyo vilithibitisha kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo.
Hakimu Bongole alisema kati ya Desemba 12 mwaka 2024 hadi Februari 10 mwaka 2025 katika maeneo ya Bomani na Mseto mkoa wa Geita mshtakiwa alikuwa akiishi na mwanafunzi huyo nyumbani kwake kama mke wake kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Aidha alisema ameangalia ushahidi wa pande zote na kubaini kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo pasipokuacha shaka yoyote, hivyo mahakama hii iinamtia hatiani mshtakiwa kwa kosa aliloshtakiwa nalo, pia mahakama hii inamtaka mshtakiwa kutoa maombolezo ya kupunguziwa adhabu.
Mshtakiwa huyo wakati wa maombolezo ya kupunguziwa adhabu aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ni kosa lake la kwanza, pia anafamilia inamtengemea.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa serikali Desideri aliomba mahakama itowe adhabu kwa mujibu wa sheria ili kukomesha vitendo vya ubakaji katika mkoa wa Geita.
Hakimu Bongole alitupilia mbali utetezi wa mshtakiwa huyo na kusema katika kosa la ubakaji ina adhabu moja tu, pia kitendo cha mshtakiwa kuchukua mwanafunzi na kuishi naye kama mke wake ni kinyume na sheria, hivyo mahakama hii inakuhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na ukimaliza kifungo chako utakuwa umejifunza namna ya kuishi na jamii. Rufaa ipo wazi kwa upande wowote ambao haujaridhika na hukumu hii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED