Bashe: Hatutazuia nchi jirani kununua mbolea ya Tanzania

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:36 PM Jun 12 2025
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Picha:Mtandao
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

Serikali imeweka wazi kuwa haitazuia nchi jirani kununua mbolea kutoka Tanzania, kwa kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kukuza biashara ya kimataifa na kusaidia wawekezaji kurudisha mitaji yao.

Aidha, imetangaza kununua tani 200,000 za mbolea kutoka kwa wazalishaji wa ndani ili kuzisambaza katika maeneo ya nchi ambayo bado yana matumizi duni ya pembejeo hiyo muhimu, ikiwa ni mkakati wa kuimarisha kilimo na kulinda uwekezaji wa viwanda vya ndani.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea nchini cha Intracom Fertilizer Ltd  kilichopo Nala, kinachotarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Juni 28, 2025. 

“Kuna mahitaji makubwa kutoka nchi jirani. Kenya tayari wameanza kuchukua mbolea, na Malawi nao wameonesha nia. Serikali haitazuia mauzo ya mbolea nje ya nchi. Hii ni biashara, na lengo ni kuhakikisha mwekezaji anarudisha mtaji wake na kulipa mikopo aliyoichukua,” amesema Bashe. 

Amefafanua kuwa uzalishaji mkubwa wa ndani unaongeza uwezo wa nchi kujitegemea kwenye pembejeo za kilimo, huku wakihamasisha matumizi ndani na kusafirisha ziada nje. 

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Intracom Fertilizer Ltd, Nduwimana Nazaire, amewahimiza wakulima kutumia mbolea zinazozalishwa nchini, kwa kuwa  wakati umefika wa kuunga mkono bidhaa za ndani zinazokuza uchumi na kuongeza ajira.

Amebainisha kuwa uwekezaji wa kiwanda hicho ni zaidi ya Dola milioni 180 za Kimarekani, ambapo sehemu kubwa ya fedha hizo zimetolewa na mabenki ya ndani na tayari kimezalisha ajira zaidi ya 1,800 za moja kwa moja, huku ajira zisizo za moja kwa moja zikikadiriwa kufikia zaidi ya 5,000, na matarajio ni kuongezeka kwa zaidi ya watu 15,000 kunufaika kiuchumi kutokana na shughuli zake.