Walimu waomba uzio wanafunzi kurubuniwa kwa pipi na kuibiwa mabegi

By Christina Haule , Nipashe
Published at 06:57 PM Jun 11 2025
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mazimbu B, Asteria Sichalwe akizungumza na mwandishi wa Nipashe hayupo pichani.
Picha:Christina Haule
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mazimbu B, Asteria Sichalwe akizungumza na mwandishi wa Nipashe hayupo pichani.

Walimu wakuu wa Shule za Msingi Mazimbu A na B, zilizopo Manispaa ya Morogoro, wameiomba Serikali kuona umuhimu wa kujengea shule hizo uzio ili kuwaepusha wanafunzi na hatari mbalimbali zikiwemo ajali za vyombo vya moto, wizi wa mabegi na upungufu wa usalama wakiwa shuleni.

Akizungumza shuleni hapo na Nipashe Digital, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazimbu B, Asteria Sichalwe, amesema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni ukosefu wa uzio, hali inayosababisha wanafunzi kuwa kwenye hatari kubwa ya kugongwa na pikipiki pamoja na bajaji zinazopita ndani ya eneo la shule hiyo.

“Mbali na ajali, pia tumekuwa na changamoto ya wizi wa mabegi ya wanafunzi. Kuna wakati mwanamke mmoja alikuwa akiwadanganya watoto kwa kuwapa pipi na pesa kidogo ili awaagize dukani, kisha anawaomba mabegi yao awakabidhiye, lakini wanaporudi wanakuta ameshaondoka,” amesema Mwalimu Sichalwe.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, shule hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa, ambapo kati ya madarasa 12 yaliyopo, manane (8) yamechakaa kiasi kwamba mvua ikinyesha wanalazimika kuwahamisha wanafunzi kwenye korido hadi mvua iishe, kisha kuendelea na masomo baada ya kutoa maji yaliyotuama.

Aidha, shule hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa madawati na matundu ya vyoo, jambo linaloathiri kwa kiasi kikubwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazimbu A, Anitha Nathan, amesema ukosefu wa uzio tayari umesababisha wanafunzi wawili wa shule hiyo kugongwa na gari wakati wakivuka barabara kuu ya lami. Amesema wanafunzi wamekuwa na uhuru wa kutoka na kuingia kwenye eneo la shule ovyo hasa nyakati za mapumziko, hali inayowaweka kwenye hatari kubwa.

Anabainisha kuwa shule hiyo pia inapokea wanafunzi wenye changamoto za afya ya akili kupitia kituo maalum kilichopo shuleni hapo, hivyo uwepo wa uzio ungewasaidia pia watoto hao kuwa salama zaidi.

“Ukosefu wa uzio unaathiri pia utulivu wa wanafunzi na unaharibu mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji. Tayari tumeanza vikao vya kupanga bajeti ili kuwasilisha maombi rasmi kwa Manispaa,” amesema Mwalimu Anitha.

Akizungumzia ombi hilo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhandisi Pascal Kihanga, amewashauri wazazi wa wanafunzi wa shule hizo kuanza kwa kushirikiana na kuanzisha ujenzi wa uzio, huku Serikali ikiahidi kuongeza nguvu baada ya hatua za awali kufanyika, kama taratibu za ujenzi wa shule zinavyoelekeza.

Shule ya Msingi Mazimbu B ni shule ya mkondo iliyoanzishwa mwaka 2008 kutokana na ongezeko la wanafunzi katika Shule ya Msingi Mazimbu A, ambapo shule hizo mbili zinashiriki eneo moja la kiwanja.