Salum Mwalimu: Wametubeza, lakini sasa hivi wanapambana na sisi

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 06:51 PM Jun 11 2025
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, amesema licha ya kubezwa na kubeukwa katika harakati zao za kisiasa, sasa wapinzani wao wanalazimika kupambana nao kwa nguvu zote.

Akizungumza wakati wa mikutano ya Oparesheni C4C inayoendelea mkoani Katavi na Tabora, Salum amesema kuwa wapinzani wao wanakaribia kuchoka huku CHAUMMA wakiendelea kuimarika.

"Wametucheka, wametubeza, lakini leo wanapambana na sisi. Tukitoka sisi, wao wanaingia. Tunawaambia wataishiwa mafuta na nguvu. Sisi (CHAUMMA) tunamaliza round hii, tunajaza mafuta, tunaingia round nyingine," amesema.

Ameeleza kuwa helikopta wanayoitumia kwa ziara hizo, baada ya kukamilisha mizunguko ya sasa, itarudi Kenya kwa matengenezo kabla ya kurejea kwa awamu nyingine ya oparesheni hiyo.

"Tunawaambia hiki chombo (helikopta), tunamaliza round hii, kinarudi Kenya kwenda kufanyiwa service, kinarudi, tunarudia round nyingine, halafu ndipo tunaingia tena kwenye kampeni," amesema Mwalimu.

Salum Mwalimu amesema mkakati wa CHAUMMA ni kutumia akili kubwa, busara na hekima kukabiliana na changamoto za kisiasa badala ya kutumia nguvu au ubabe wa maneno.

"Tunahitaji busara kwenye nyakati ngumu, siyo ubabe. Tunahitaji akili kubwa kwenye nyakati ngumu na siyo ubabe. Tumekataa ubabe usioendana na hekima na busara. Unapokuwa na misimamo mikali, lazima uwe na mikakati na akili kubwa ya kutekeleza hiyo misimamo," amesisitiza.

Ameongeza kuwa katika nyakati ngumu, kinachotakiwa siyo papara wala jazba, bali utulivu na mipango madhubuti, akisema: "Akili kubwa, hekima, busara, utulivu – vinahitajika kwenye nyakati ngumu, siyo papara, siyo maneno. Ndio maana Mwenyezi Mungu anasema kiungo cha kukiogopa kuliko vyote ni ulimi."

CHAUMMA inaendelea na Oparesheni C4C iliyozinduliwa rasmi Juni 3, 2025, jijini Mwanza, ambapo kwa sasa mikutano inafanyika mkoani Katavi na Tabora kwa kutumia helikopta maalum.