Rais wa Shule ya Utawala Afrika (ASG), Profesa Kingsley Moghalu, amesema changamoto za utawala Afrika haziwezi kutatuliwa kwa kutumia mifumo ya kuagizwa kutoka nje.
Akizungumza katika ziara yake aliyoifanya katika miji ya Nairobi nchini Kenya, Lagos, Cairo, Maputo na Abidjan, alisema kutokana na hali hiyo kutaundwa kitu kipya ambacho kimebuniwa na Afrika kwa ajili ya Afrika.
Katika kuhakikisha waafrika wengi wanapata nafasi, ASG ina mpango wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu hiyo kote barani Afrika.
Prof.Moghalu alisema ifikapo mwaka 2027, ASG itaongeza kozi nyingine katika maeneo ya utawala wa makampuni na fedha za umma.
Prof. Moghalu ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria, anaongoza taasisi hiyo akiwa na dira ya kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi za Afrika.
“Huu ni mwanzo wa kitu chenye nguvu, ASG ndiyo chimbuko la mustakabali wa utawala bora Afrika," alisema Prof.Moghalu.
Katika ziara yake hiyo kwenye miji mikuu ya Afrika imeashiria mwanzo wa zama mpya katika elimu ya uongozi na utawala barani Afrika.
Ziara hiyo ilivuta hisia kubwa kutoka kwa viongozi wa serikali, watunga sera, wasomi, washirika wa maendeleo na vijana wanaotamani kuwa viongozi wa mabadiliko.
Katika kilele cha Mkutano wa Utawala wa Nairobi, Profesa Moghalu alisema kwa msisitizo: “Swali halitakuwa ulisoma nini au wapi. Katika miaka kumi ijayo, swali litakuwa: je, umejiunga na ASG?”
Aidha, ASG imezindua rasmi Mpango wa Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma (MPA) unaotarajiwa kuanza Septemba 2025, kwa ushirikiano na Taasisi mashuhuri ya Lee Kuan Yew School of Public Policy, Chuo Kikuu cha Taifa cha Singapore.
Mtaala wa mpango huu umebuniwa kwa kuzingatia uhalisia wa Kiafrika, ukilenga kuibua uongozi wa kimaadili, kiutendaji na wa mabadiliko.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED