Mwanachuo mbaroni madai ya kumuua mwenzake

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 04:16 PM Jun 17 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamini Kuzaga.

Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ( MUST), Emilian Duzu (21) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzake wa Chuo hicho mwaka wa tatu aitwaye Gerald Said (22).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamini Kuzaga amethibisha tukio hilo leo June 17, 2025 alipozungumza na Waandishi wa Habari.

Amesema   Juni 14, 2025  majira ya saa 11 alfajiri   kwenye   klabu  iitwayo Mbeya Pazuri iliyopo jijini Mbeya,  mtuhumiwa Duzu alimjeruhi  Said  kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni hali iliyosababisha  kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu lakini ilipofika saa saba mchana alifariki dunia.
 
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokana na ulevi wa kupindukia wakiwa eneo la ndani la klabu hiyo ambapo mabaunsa waliwaamua na ndipo mtuhumiwa alitokanje na kuelekea eneo la maegesho alipokuwa ameegesha gari, marehemu alimfuata kwa lengo la kuendelea kugombana ndipo mtuhumiwa alimchoma  na kitu chenye ncha kali,” ameeleza  Kamanda Kuzaga.
 
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito  kwa wanafunzi  kuzingatia masomo na kujiepusha na vitendo visivyofaa ikiwemo ulevi wa kupindukia kwanini hatari kwa afya zao na maisha yao.