Vijana wanne wachomwa moto Kahama tuhuma za uhalifu

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 07:24 PM Jun 17 2025
 Vijana wanne wachomwa moto Kahama tuhuma za uhalifu
Picha: Mpigapicha Wetu
Vijana wanne wachomwa moto Kahama tuhuma za uhalifu

Vijana wanne wasiojulikana majina yao wala makazi wameuawa kwa kupigwa na kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali katika Mtaa wa Mhongolo, Kata ya Mhongolo, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uhalifu na uporaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa vijana hao waliuawa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi. Polisi walifika eneo la tukio na kuchukua miili ya marehemu, ambayo imehifadhiwa katika hospitali ya Manispaa ya Kahama.

Kamanda Magomi alisema wahalifu hao walipigwa kwa mawe sehemu mbalimbali za miili yao kabla ya kuchomwa moto. Hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

Amesikitishwa na kitendo hicho, akisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na hakuna aliye juu ya sheria, akiwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.

“Tutafanya msako mkali nyumba kwa nyumba ili kuwatambua waliohusika. Tukiruhusu tabia hii iendelee, hakutakuwa na amani. Kila mmoja atakuwa mtoa haki kwa mujibu wa anavyotaka,” alisema Magomi.

Aliongeza kuwa hata kama mtu ni mkosaji au mtuhumiwa wa wizi, alipaswa kukamatwa na kufikishwa polisi kwa hatua zaidi za kisheria, badala ya kuuawa bila kupitia kwenye vyombo vya haki.

Kwa upande wake, mkazi wa Kata ya Mhongolo, Juma Samweli, alikemea kitendo hicho akisema wananchi walipaswa kutoa taarifa polisi badala ya kujichukulia sheria mkononi. Aliahidi kushirikiana na vyombo vya dola kuwabaini waliohusika ili tabia hiyo ikomeshwe.

Aidha, Samweli aliitaka serikali kuimarisha ulinzi katika maeneo hatarishi, akitaja miti ya miembe na nyumba ambazo hazijakamilika ujenzi wake kuwa maficho ya wahalifu wanaopora wananchi.

Naye Mwasiti Hamisi, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, alisema alitoka kazini na kukuta umati wa watu katika eneo la tukio, na kuelezwa kuwa vijana hao walipigwa mawe na kuchomwa moto kwa tuhuma za kuwanyang’anya wananchi fedha, simu na mikoba kwa kutumia mapanga na marungu.