Serikali kuboresha Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani kwa ngazi ya Kimataifa

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 04:27 PM Jun 17 2025
Serikali kuboresha Kituo cha  Mafunzo ya Ulinzi wa Amani  kwa ngazi ya Kimataifa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Serikali kuboresha Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani kwa ngazi ya Kimataifa.

Serikali imetangaza mpango wa kuimarisha mchango wake katika juhudi za kulinda amani duniani kwa kukiboresha Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Tanzania (TPTC) ili kiweze kutoa mafunzo kwa ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mkuu wa Jeshi la Anga  Meja Jenerali Shabani Mani alisema hayo Jijini Dar.es.salaam mwishoni mwa wiki  alipokuwa akifunga  mafunzo ya kwanza kabisa ya raia kuhusu ulinzi wa amani yaliyofanyika katika kituo hicho.

Meja Jenerali Mani alimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, ambaye hakuweza kuhudhuria kutokana na majukumu mengine ya kikazi.

Alisema kuwa maboresho hayo yataifanya TPTC kuwa kitovu muhimu cha mafunzo ya vipengele vyote vitatu vya operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa: jeshi, polisi na raia.

Alisisitiza kuwa kituo hicho kitakapoboreshwa kitaweza kuandaa vikosi kamili vya ulinzi wa amani vilivyofunzwa kwa kiwango cha juu na tayari kwa misheni mbalimbali duniani.

Aidha, alieleza kuwa kituo hicho kinatarajia kuanzisha kozi mpya zinazolenga kujenga uwezo wa Watanzania, wakiwemo raia, ili waweze kushiriki ipasavyo katika juhudi za kulinda amani duniani.

“Mafunzo haya ya mwanzo ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania kwenye ulinzi wa amani. Yanalenga kuhakikisha kuwa kila anayeshiriki katika misheni anakidhi viwango vya kimataifa,” alisema.

Aliongeza kuwa huu ni mwanzo tu wa mpango mpana zaidi, na kwamba mafunzo mengine yatafuata hivi karibuni.

Kwa upande wake, Kamanda wa TPTC, Brigedia Jenerali George Itang’are, alisema kuwa mafunzo hayo yamefanyika kwa ushirikiano na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Mpango wa Maendeleo la  Umoja wa Mataifa (UNDP).

“Tunafurahi kuona raia wakionyesha hamasa ya kujifunza jinsi vipengele mbalimbali vya ulinzi wa amani vinavyofanya kazi. Aidha, mafunzo haya pia yalihusisha askari polisi waliovaa sare,” alieleza.

Nomula Hiroyuki, mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Tanzania, alieleza kuwa Japan inajivunia kusaidia mpango huo kama sehemu ya kujitolea kwake katika kuendeleza amani duniani na kuinua jamii.

“Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na dhamira ya pamoja, hata mataifa ya mbali kama Japan yanaweza kuwa na mchango chanya katika maeneo ya ndani kama haya,” alisema.

“Kwa kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Mataifa pamoja na wadau mbalimbali, tumeweka juhudi mahususi kuunga mkono na kuendeleza jitihada zenye mafanikio,” aliongeza.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP John Rutele alisema kuwa programu hizi za mafunzo zitasaidia kuongeza mchango wa Tanzania katika operesheni za kimataifa za ulinzi wa amani na kuiimarisha nafasi yake kimataifa.

Alisema  kuwa Tanzania inaendelea kufanya maendeleo makubwa, na kwamba UNDP inaiona nchi hiyo kama kinara anayeibuka katika ulinzi wa amani ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Rutele alisisitiza pia umuhimu wa kuendeleza ushirikiano na washirika wa maendeleo ili kuendeleza na kupanua programu za mafunzo, ikiwa ni pamoja na kuwakaribisha washiriki kutoka nchi jirani.

“UNDP imejidhatiti kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kuimarisha amani endelevu na maendeleo, kuhakikisha kuwa Watanzania wanakuwa na uwezo wa kuchangia kikamilifu katika utulivu wa kikanda na kimataifa,” alisema kwa msisitizo.

Nice Munis, Afisa wa Masuala ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema “Majukumu yetu yanahusisha utekelezaji wa sera ya mambo ya nje, ikiwa ni pamoja na kuimarisha amani na usalama – jambo ambalo linagusa maslahi ya kila taifa duniani.”

“Mafunzo haya yamenipa uelewa mpana na kunitia nguvu. Nimegundua kwamba hata sisi raia, licha ya kutokuwa sehemu ya vyombo vya ulinzi na usalama, tunaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi wa amani, hasa tunapotumwa kwenye misheni za kimataifa.”

“Tumezaliwa na kulelewa hapa Tanzania, hatujawahi kupitia vita kwa moja kwa moja, lakini tunasikia kutoka kwa waliopitia hali hizo.”

Aliongeza kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwa muda mrefu katika kusaidia nchi zilizoathiriwa na migogoro, kwa lengo la kurejesha na kudumisha amani.