CBE yaandaa kongamano kuwakwamua vijana na tatizo la ajira

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:00 PM Jun 17 2025
 Mkuu wa chuo hicho, Prof Edda Lwoga
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa chuo hicho, Prof Edda Lwoga

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kimeandaa kongamano la kuimarisha fursa za ajira na maendeleo endelevu linalolenga kuwawezesha vijana kujiajiri.

Hayo yamesemwa  jijini Dar es salaam na Mkuu wa chuo hicho, Prof Edda Lwoga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo litakalofanyika Alhamisi chuoni hapo. 

Amesema mgeni rasmi katika Kongamano hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo  akiambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka Serikalini na Sekta Binafsi.

“Lengo kuu la kongamano hili ni kuandaa jukwaa rasmi kwa wanafunzi wetu kuonyesha kwa vitendo yale waliyojifunza, na kuwapa nafasi ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwa waajiri na wadau mbalimbali wa maendeleo,” amesema. 

“Hii ni sehemu ya jitihada za CBE katika kushiriki kikamilifu kutafuta suluhisho la changamoto ya ajira nchini na kwa  mwaka huu, tunatarajia kuwa na zaidi ya kampuni na taasisi 30 kutoka sekta mbalimbali zitakazoshiriki kongamano hili,” amesema

 Amesema baaadhi ya taasisi zitakazoshiriki kongamano hilo ni Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), UTT AMIS na Tanzania Youth Coalition 

 ·         Ametaja taasisi zingine kuwa ni Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba Muhimbili (MUHAS).

  “Kampuni hizi zitashiriki kwa njia ya maonyesho ya wazi (Exhibition), kutoa ushauri, kuwasikiliza wanafunzi na kutoa uzoefu wa moja kwa moja kuhusu mazingira halisi ya kazi,” amesema.

 “Kongamano hili ni zaidi ya tukio la siku moja na CBE tunadhamiria kuligeuza kuwa jukwaa la kitaifa, linalowaleta pamoja wahitimu, waajiri, taasisi za serikali, sekta binafsi, na vyombo vya sera kwa lengo la kujenga mustakabali bora wa ajira na maendeleo nchini,” amesema.

 Aidha, amesema Chuo cha Elimu ya Biashara kiko tayari kuwa mshirika mkuu wa mabadiliko hayo ya kijamii na kiuchumi, kwa kutumia majukwaa hayo kuunganisha taaluma, ubunifu, ujasiriamali na fursa halisi za ajira.

 “Kwa niaba ya uongozi wa CBE, nawatakarikaribisha kwa dhati wawekezaji, waajiri, wajasiriamali, taasisi za elimu, wanafunzi na wananchi wote kwa ujumla, kuja kushiriki nasi katika kongamano hili muhimu,” amesema.

 Amesema CBE ina dhamira ya kuendelea kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, weledi, ubunifu na uwezo wa kujitegemea kwa ajili ya maendeleo endelevu ya taifa letu.

 Amesema katika kufanikisha azma hiyo chuo kilianzisha program atamizi ya biashara ambapo wanafunzi husajili mawazo yao ya biashara na kisha chuo kuwafundisha namna ya kufanikisha ndoto zao.

 Amesema nia ni kuwawezesha wahitimu wa chuo hicho kuwa na kitu cha kufanya wanapohitimu masomo yao badala ya kuhangaika kutafuta ajira kwenye kampuni mbalimbali.

 Amesema hadi sasa mamia ya wanafunzi wameshanufaika na program hiyo kwa kusimamiwa mawazo yao ya biashara ambapo waliendelea na biashara hizo baada ya kuhitimu.

 Amesema program ya uanagenzi nayo imekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi wa chuo hicho kwani wamekuwa wakisoma kwa vitendo zaidi badala ya kusoma nadharia pekee.

Amesema kupitia program hiyo ya uanagenzi wanafunzi wa chuo hicho wanatumia nusu ya muda wao wa masomo darasani na nusu ya muda kwa waaajiri mbalimbali kujifunza kwa vitendo.

Amesema CBE imeingia makubaliano na taasisi na kampuni mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukua wanafunzi hao kwenda kujifunza kwa vitendo wakiwa wanaendelea na masomo chuoni hapo. 

“Hii inamsaidia mwanafunzi kuajirika mara tu anapomaliza masomo yake kwakuwa anakuwa na ujuzi ambao ameupata anaposoma kwa vitendo badala ya kubaki na nadharia ya darasani pekee,” amesema Prof Edda.