Mwenyekiti wa Kamati ya Mapambano dhidi ya Vishoka katika taaluma ya sheria, Wakili Sweetbrt Nkuba amewataka wananchi kutumia huduma za mawakili waliothibitishwa ili kuepuka kushawishiwa na watu wanaotoa huduma kwa bei rahisi.
Aidha, amesema mashirika ya umma na binafsi yashirikiane na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika kuwakagua wanaojihusisha na kazi za kisheria ili kutokomeza kabisa vishoka katika taaluma ya sheria.
Nkuba amesema hayo leo Juni 17, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza vishoka wa uwakili nchini na kuhusu malipo ya mawakili kwa sababu changamoto ya vishokoa imekuwa kubwa.
"Kwa masikitiko makubwa, tumeshuhudia ongezeko la watu wanaojihusisha na
utoaji wa huduma za kisheria bila kuwa mawakili. Hawa huitwa vishoka na matendo yao ni kinyume cha sheria," amesema Nkuba
Amesema wanachama wasiohuisha leseni zao na waliojisajili kutotoa huduma (Non-Practicing Members) hao ni watu waliowahi kuwa mawakili lakini hawajasajiliwa au kuhuisha leseni za uwakili kwa mwaka husika, au wameomba
kwa kipindi fulani.
" Au wamefungiwa kutoa huduma lakini wao wanaendelea kutoa huduma hizi, kujihusisha kwao na huduma za uWakili bila uhalali ni kinyume cha sheria. Pia wanatumia mihuri bandia au kughushi mihuri ya mawakili halali ili uwadanganya wananchi,"
"Kitendo hiki ni kosa la jinai linaloathiri uaminifu wa nyaraka za kisheria. Kumekuwa na wimbi la mawakili wasio waaminifu wanaoruhusu watu wasio mawakili kutumia mihuri yao kuthibitishia nyaraka au kutoa viapo," Amesema Nkuba
Amesema kuwa suala hilo ili limesababisha kuwepo na wimbi la wahalifu kuchonga mihuri na
kuitumia kama mawakili, hilo wanalishuhudia katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za Serikali zinazohitaji huduma ya mawakili kama Uhamiaji, NIDA na ofisi zingine.
"Tunapenda kuwakumbusha wananchi kuwa nyaraka yoyote iliyowekwa muhuri wakili na mtu asiye wakili kuwa nyaraka hiyo ni ya kughushi na ni batili iwe kiapo au mkataba, mnatakiwa muende kwa mawakili husika,"
"Baadhi ya wananchi wengi wapo tayari kumlipa dalali hadi asilimia 10 bei ya manunuzi ya nyumba/kiwanja lakini kutoa asilimia tatu au sita kwa wakili kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa huonekana kama sio stahili wakati wakili ndiye anayehalalisha makubaliano husika,"Amesema Nkuba
Pia, Nkuba ameziomba mamlaka za usalama ziongeze juhudi katika kuwakamata na kuwafungulia mashtaka vishoka na pia wananchi watoe taarifa kuhusu watu wanaotoa huduma za kisheria bila usajili au kwa kutumia nyaraka bandia.
Amesema tabia hizo potofu zinaathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya taaluma ya sheria na taifa kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED